Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka wadau wa Elimu kuhakikisha
wanatumia takwimu sahihi zilizotolewa na Mamlaka husika wakati wa kuandaa machapisho
yao ili kuepuka kupotosha umma.
Waziri Ndalichako amesema
hayo leo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa kutathmini Sekta ya Elimu
unaoshirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi kuwa kipaumbele cha Serikali ya
awamu ya Tano ni Elimu na ndio maana Wizara hiyo imekuwa ikitengewa bajeti ya
kutosha na bajeti ya Wizara hiyo haijawahi kushuka.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akifungua Mkutano Mkuu
wa mwaka wa kutathmini Sekta ya Elimu uliofanyika Jijini Dodoma. Waziri
Ndalichako amewataka washiriki wa mkutano huo kujadili kwa kina mafanikio,
changamoto na kuwa na mikakati ya pamoja itakayosaidia Serikali kufikia malengo
waliojiwekea katika Sekta ya Elimu.
Waziri Ndalichako amesema
kumekuwa na upotoshwaji wa takwimu zinazotolewa kwenye machapisho mbalimbali
kuwa bajeti ya Wizara ya Elimu imeshuka hadi kufikia asimilia 56 suala ambalo
Waziri Ndalichako amelikanusha na kueleza kuwa bajeti ya Wizara hiyo haijawahi
kushuka na mpaka Juni 2018 bajeti ya Wizara hiyo ni asilimia 86.5.
“Bajeti ya Wizara ya Elimu
haijawahi kushuka kwa kuwa kipaumbele cha serikali ya awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais John Magufuli ni Elimu, hivyo takwimu ambazo zimekuwa
zikitolewa kwenye machapisho mbalimbali sio sahihi na badala yake takwimu sahihi za bajeti ya
Wizara ya Elimu ni asilimia 86.5 hadi kufikia Juni 2018,” alisisitiza Waziri
Ndalichako.
Katibu
Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo akizungumza
wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa kutathmini Sekta ya Elimu unaofanyika
Jijini Dodoma.
Waziri Ndalichako amewaambia
wadau wa Mkutano huo wa AJESR unaofanyika Jijini Dodoma kuwa Elimu ndio nyenzo
muhimu inayotoa dira na muongozo ili kuhakikisha Taifa linakuwa na watu
walioelimika kwa maendeleo ya Taifa katika kufikia uchumi wa viwanda na uchumi
wa kati ifikapo 2025.
Waziri Ndalichako amewataka
washiriki wa mkutano huo kujadili kwa kina mafanikio, changamoto na kuwa na
mikakati ya pamoja itakayosaidia Serikali kufikia malengo waliojiwekea katika
Sekta ya Elimu.
Wadau
wa Elimu walioshiriki Mkutano Mkuu wa mwaka wa kutathmini Sekta ya Elimu
wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce
Ndalichako wakati wa Ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika Jijini Dodoma.
Mkutano huo wa mwaka wa
kutathmini Sekta ya Elimu umekuwa
ukishirikisha wadau mbambali wa ndani nan je ya nchi ulianza mwaka 2008 na umekuwa ukifanyika kila
mwaka.
Kauli mbiu ya Mkutano huo ni
“Upatikanaji wa Elimu bora kufikia
Tanzania ya Viwanda” umeanza leo na utakamilika
Septemba 28, 2018.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.