Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhe. William Ole Nasha ameitaka Mamlaka ya Elimu Tanzania, (TEA)
kuanza kutumia utaratibu wa Force Akaunti katika utekelezaji wa
miradi ya Elimu wanayoisimamia kwa kuwa utaratibu huo unawezesha kazi
kukamilika kwa wakati, lakini pia kujenga majengo yenye
ubora kwa gharama nafuu.
Ole Nasha ametoa agizo hilo
mkoani Manyara wakati akikagua shughuli za ujenzi katika shule ya
Sekondari ya wasichana Nangwa na ile ya Endasak zilizopo Wilayani Hanang
ambazo kwa pamoja ujenzi wake unatekelezwa na Wizara hiyo kupitia Programu
ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) na Mamlaka ya Elimu Tanzania.
“Nitawapeni mfano Shule ya
Sekondari Endasak imejengewa bweni na Wizara ya Elimu kupitia Mamlaka ya
Elimu Tanzania lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kwa zaidi ya
shilingi milioni 170, huku miradi mingine inayotekelezwa na Wizara kupitia
Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) ikitumia kiasi hicho hicho kujenga
mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kila
moja kwa utaratibu wa Force Akaunti,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipata maelezo ya
maendeleo ya ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya wasichana Nangwa
kutoka kwa Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang Sembua Faraja. Shule
hiyo iko katika Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara.
Kiongozi huyo
amesema mahitaji ya Taifa letu kwenye Sekta ya Elimu bado ni makubwa
hivyo ni vizuri kurudi katika utaratibu wa kutumia Force Akaunti ili
kuweza kuwapatia malazi wanafunzi wengi pamoja na kutatua changamoto nyingine
zilizopo kwenye Sekta ya Elimu.
Naibu Waziri huyo pia amewaagiza
viongozi wa elimu mkoa wa Manyara kuhakikisha Shule ya Sekondari ya
Endasak katika mwaka wa masomo 2019/20 inapangiwa wanafunzi wa kidato
cha tano kwa kuwa tayari ina miundombinu inayotosheleza
likiwemo bweni lililojengwa na Wizara hiyo.
Muonekano
wa nje wa bweni lililojengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia
Mamlaka ya Elimu Tanzania katika shule ya sekondari Endasak iliyoko katika Wilaya
ya Hanang mkoani Manyara.
Akizungunza na
wanafunzi wa Shule ya
Sekondari ya wasichana Nangwa na ile
ya Endasak Mheshimiwa Ole Nasha amewataka wanafunzi
hao kuwa na bidii katika masomo, waadilifu lakini pia kuwa wazalendo kwa
nchi yao kwani kwa kufanya hivyo wataweza kuitetea nchi yao na
kutoshiriki katika vitendo viovu.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiongea na wanafunzi
katika shule ya Sekondari ya Wasichana Nangwa iliyoko katika Wilaya ya Hanang
Mkoani Manyara. Amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii, kuwa waadilifu na wenye
uzalendo katika nchi yao ili kuepuka kujiingiza katika vitendo viovu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.