Ijumaa, 23 Novemba 2018

OLE NASHA: SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA WAHISANI KATIKA SEKTA YA ELIMU


Serikali imesema inatambua mchango wa wahisani na wadau wa Elimu katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Tano katika kuendelea kuchangia ujenzi wa mabweni ya Wanafunzi wa kike, ujenzi wa vyumba vya madarasa, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA pamoja na ununuzi wa vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.William Ole Nasha wakati akitunuku hati za utambuzi kwa Wahisani na Wadau ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia Miradi ya Elimu kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwenye hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akimkabidhi hati ya utambuzi kwa mchangiaji wa Miradi ya Elimu Kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo Naibu Waziri Ole Nasha amewahakikishia wahisani hao usalama wa fedha zao na kuwa zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

“Niwahakikishie kuwa Serikali inatambua mchango wenu katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuchangia Elimu, ikiwa ni pamoja na kuchangia ujenzi wa mabweni ya Wanafunzi wa kike, ujenzi wa vyumba vya madarasa, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA pamoja na ununuzi wa vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum,”

“Pia fedha zilizotolewa na Taasisi zenu zitatumika kama zilivyokusudiwa na si vinginevyo na endapo itabainika kuwepo kwa matumizi ambayo siyo sahihi basi Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote watakaobanika kwenda kinyume na maelekezo”alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.
Wachangiaji wa Miradi ya Elimu kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia Mhe. William Ole Nasha  mara baada ya wahisani hao kutunukiwa hati za utambuzi.

Jumla ya Taasisi 18 za ndani na nje ya nchi zilitunukiwa hati baada ya kuchangia takribani Shilingi  bilioni 11  ambazo zimetumika kuboresha Miundombinu mbalimbali ya Elimu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.