Jumatatu, 26 Novemba 2018

TANZANIA NA CHINA ZATILIANA SAINI KUANZA UJENZI WA CHUO CHA VETA KAGERA


Serikali ya Tanzania na ile ya Jamuhuri ya watu wa China leo zimetiliana  saini makubaliano ya kuanza kwa ujenzi wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ambacho kinatarajiwa kujengwa mkoani Kagera na kuwa ujenzi huo unatarajiwa  kukamilika mwaka 2020

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leornald Akwilapo ndiye aliyesaini mkataba huo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na  kwa upande wa China mkataba huo umesainiwa na Mwakilishi wa Uchumi na Biashara nchini Tanzania Yuan Lin na kuwa tukio hilo limefanyikia jijini Dar es salaam.


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leornald Akwilapo pamoja na Mwakilishi wa Uchumi na Biashara nchini Tanzania Yuan Lin wakitia saini  mkataba wa makubaliano wa ujenzi wa chuo cha VETA kinachotarajiwa kujengwa mkoani Kagera na ujenzi wake  unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.

Mara baada ya kusaini mkataba huo Dkt. Akwilapo amesema kuwa Chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 wa kozi za muda mrefu na wanafunzi  1000 wa kozi za muda.

Miundombinu itakayojengwa katika chuo hicho ni pamoja na vyumba vya madarasa, Karakana za Kufundishia, Majengo ya Utawala, mabweni  na Viwanja vya michezo na kuwa mpaka kukamilika kitagharimu zaidi ya shilingi bilioni 22.

 Dkt. Akwilapo amewataka wakandarasi  wanaopewa mikataba ya ujenzi na Wizara yake kuhakikisha wanatekeleza makubaliana ya mikataba hiyo kwa wakati  na kwamba serikali haitasita kuvunja mkataba wowote ambao unatekelezwa kinyume na makubalino ikiwa ni pamoja na  kuchukulia hatua za kisheria kwa kwenda kinyume na mikataba hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leornald Akwilapo pamoja na Mwakilishi wa Uchumi na Biashara nchini Tanzania Yuan Lin wakibadilisha hati za mkataba wa makubaliano ya ujenzi wa chuo cha VETA kinachotarajiwa kujengwa mkoani Kagera.



Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema Chuo hicho kitasaidia kuongeza udahili wa wanafunzi katika fani mbalimbali za VETA kutokana na ukweli kwamba mkoa huo ni mkubwa na kuwa hapo awali ulikuwa na chuo cha VETA kimoja kinachojulikana kama Rwamishenye ambacho kilikuwa kidogo.

Naye Mwakilishi wa China anayeshughulikia masuala ya Uchumi na Biashara nchini Tanzania Yuan Lin amesema Serikali ya Tanzania na China zimekuwa marafiki kwa muda mrefu na ndio maana China imeona umuhimu wa kusaidia ujenzi wa chuo hicho ikiwa ni hatua ya kuunga mkono Juhudi za Serikali ya awamu ya Tano ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda hadi ifikapo mwaka 2020.

Katibu Mkuu Waizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leornald Akwilapo akisoma mkataba wa makubaliano wa ujenzi wa chuo cha VETA kinachotarajiwa kujengwa mkoani Kagera.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni