Jumamosi, 24 Novemba 2018

WAZIRI NDALICHAKO ASEMA AFRIKA ITAENDELEZWA NA WAAFRIKA WENYEWE


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema wajibu wa kuiendeleza Afrika uko mikononi mwa Waafrika wenyewe huku jukumu la wadau wengine wa Maendeleo ni  kusaidia kukua kwa Maendeleo hayo.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo Leo katika Mahafali ya Programu za ESAMI yaliyofanyika katika Makao Makuu ya ESAMI jijini Arusha ambapo amesisitiza kuwa  Waafrika wanapaswa kujisimamia wenyewe katika nyanja za Kijamii na Kiuchumi  kwa lengo la kutimiza malengo ya bara hilo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa kozi za ESAMI katika Mahafali yaliyofanyika jijini Arusha

“ Ili Afrika iweze kuendelea lazima ijisimamie yenyewe katika masuala ya kijamii na kiuchumi na hii itawezekana tu kupitia   vijana ambao wameandaliwa  vyema na wakawa tayari kuhakikisha wanaliendeleza bara la Afrika kwa ujasiri bila kuhofia changamoto watakazokutana nazo,” alisisitiza Waziri Ndalichako

Kiongozi huyo amesema bara la Afrika linahitaji Viongozi wenye ujasiri, ambao wapo tayari kuhakikisha Afrika inakwenda mbele kiuchumi na Kijamii.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika maandamano ya kitaaluma wakati wa mahafali ya Programu za ESAMI yaliyofanyika katika Makao Makuu ya ESAMI jijini Arusha

Akizungumza katika mahafali hayo Mkurugenzi Mkuu wa ESAMI Prof. Bonard  Mwape amesema wahitimu wote wameandaliwa vyema kwenda kuleta Mabadiliko  na Maendeleo katika nchi zao pamoja na kuhakikisha  bara la Afrika linakuwa  lenye maendeleo.

Mahafali hayo yamejumuisha zaidi ya wahitimu 360 kutoka nchi za Afrika ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Namibia, Mali, Malawi DR- Congo, Burundi, Zimbambwe na wenyeji Tanzania.

Baadhi ya wahitimu wa kozi mbalimbali wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia (Hayupo Pichani) wakati wa mahafali wakati wa mahafali ya Programu za ESAMI yaliyofanyika katika Makao Makuu ya ESAMI jijini Arusha

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.