Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William
Ole Nasha amesema ni kosa kusambaza nyaraka za serikali katika mitandao ya
kijamii bila idhini ya Mamlaka husika, hivyo ameagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu
na za kisheria kwa watumishi watakaobainika kusambaza nyaraka hizo.
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo mkoani Morogoro wakati akifunga
semina ya mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu kwa baadhi ya Maafisa
wa Wizara hiyo na kusisitiza kuwa hakuna mtumishi yeyote wa serikali asiyefahamu
kuwa kutoa nyaraka za serikali bila idhini ni kosa la jinai.
“Kumekuwa na usambazaji wa nyaraka za serikali katika mitandao ya
kijamii bila idhini na kwa bahati mbaya wakati mwingine unakuta nyaraka imewekwa
mhuri wa siri lakini bado unaikuta huko, watumishi wa serikali lazima watambue kuwa
kuna utaratibu wa kutoa nyaraka za serikali na kuna sheria ambazo zinawabana wale
wote wanaotoa taarifa hizo bila kuidhinishwa”alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akizungumza na washiriki wa Wizara hiyo (hawapo
Pichani) waliohudhuria mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu ambayo
yamekamilika leo mkoani Morogoro.
Mhe. Ole Nasha amewataka watumishi hao kutambua kuwa hakuna taasisi
yeyote inayoweza kufanya kazi bila kuwa na kumbukumbu au nyaraka hivyo amewataka
kuhakiksha utunzaji mzuri na salama wa nyaraka hizo kwani ni nguzo muhimu katika
kufanikisha utendaji wa majukumu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali watu, Moshi Kabengwe amesema
mafunzo hayo yametolewa ili kusaidia watumishi kufanya kazi ambazo zitaleta tija
kwa jamii inayohudumiwa na kuondoa changamoto ambazo zimebainika katika utoaji wa
huduma.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William
Ole Nasha akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa mafunzo ya siku tano ya Huduma
kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu ambayo yamefungwa leo mkoani Morogoro.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku
tano na yameshirikisha watumishi zaidi ya 50 kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Makao Makuu, Vyuo vya Ualimu vilivyopo Morogoro na baadhi ya watumishi
kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiwa katika picha ya
pamoja na washiriki wa mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.