Jumatano, 30 Januari 2019

WAZIRI NDALICHAKO ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA CHUO CHA VETA WILAYANI CHATO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako leo ameendelea na ziara yake mkoani Geita ambapo ametembelea mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA kinachojengwa Wilayani Chato mkoani humo na kusema kuwa ameridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa Chuo hicho Waziri amesema  upo upungufu  wa vyuo vya kutolea mafunzo ya Ufundi na tayari serikali imeendelea kujenga ili kuhakikisha dhamira ya kuwa nchi ya viwanda inafikiwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Udundi Stadi cha VETA, Wilayani Chato mkoani Geita, akiwa katika ukaguzi huo waziri alisema ameridhishwa na hatua ya ujenzi uliofikiwa.

Waziri Ndalichako ameendelea kuitaka Idara ya manunuzi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha inafanya uchaguzi sahihi wa mkandarasi na kuwa hilo ndiyo suluhisho la kukamilisha miradi ya ujenzi kwa wakati.

 “Nitumie fursa hii kuzielekeza halmashauri zote nchini kuendelea kukamilisha  majengo na majengo yakishakamilika  basi Wizara tutanunua vifaa kupitia mradi wa kukuza ujuzi na kazi (ESPJ) lengo la serikali  ni kuendeleza ujuzi ili kupata wataalamu wa kutosha,” alisema Prof. Ndalichako.
Muonekano wa moja ya jengo la chuo cha Ufundi Stadi VETA, Wilayani Chato mkoani Geita.

Akiwa Wilayani Chato, Waziri Ndalichako alizungumza na wanafunzi wa kidato cha tano na sita wa shule ya sekondari  ya wasichana ya Jikomboe ambapo ameahidi kutoa kiasi cha Tsh. Milioni mia mbili kwa ajili ya kujenga bwalo, chumba cha darasa na kumalizia uzio wa shule hiyo.

 Waziri Ndalichako kesho ataendelea na ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya ujenzi ya vyuo vya Ufundi stadi mkoani Kagera.
Muonekano wa jengo lingine katika mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA, Wilayani Chato mkoani Geita.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni