Jumamosi, 9 Machi 2019

WIZARA YA ELIMU YAGAWA KOMPYUTA 300 KWA VYUO VYA ELIMU VYA UMMA


Kiasi Cha Shilingi bilioni 1.2 kimetumika  kununulia vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya vyuo vya ualimu vya umma  18, kwa  lengo la   kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji katika vyuo hivyo ili  kuzalisha walimu bora  na wanaoendana na ulimwengu wa Teknolojia.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu Profesa James Mdoe kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati wa halfa ya utoaji vifaa mbalimbali vya TEHAMA zikiwemo Kompyuta 300, UPS 300 na Projector 100 kwa ajili  vyuo hivyo vya Ualimu.

Kaimu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe akigawa vifaa vya Tehama kwa Wakuu wa Vyuo vya Ualimu vya Umma nchini kwa lengo la kuboresha elimu ya Ualimu, hafla hiyo imefanyikia mkoani Dodoma.

Katika hotuba yake, Profesa Mdoe amesema serikali ya Tanzania inawashukuru  washiriki wa maendeleo ambao ni serikali ya CANADA kwa kufadhili mradi wa kuendeleza na kuboresha Elimu ya Ualimu  (TESP ) kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Profesa Mdoe pia amewaasa Wakuu wa Vyuo kutumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyo kusudiwa na ametoa onyo kwa Wakuu wa vyuo wote wanauhujumu jitihada za serikali za kuboresha miundombinu ya vyuo vya Ualimu kuacha mara moja tabia hiyo na kuwataka watumishi wote  kutanguliza maslahi ya Taifa ikiwa ni pamoja na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

 
Vifaa mbalimbali vya Tehama zikiwemo Kompyuta, UPS na Projector kwa ajili ya kugawiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya umma 18.

“Nipende kuwasihi watumishi wote wa Wizara ya Elimu na hasa Idara ya manunuzi   kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni  wakati wa kutekeleza majukumu."

Vyuo vya Ualimu vya Umma ambavyo vimepata vifaa hivyo ni pamoja na Dawaka, Ilonga, Mandaka, Mhonda, Murutunguru, Mamire, Ndala, Singachini, Shinyanga na Vikindu.

Kaimu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe akizungumza na watumishi wa Wizara (hawapo) pichani wakati wa hafla ya kugawa vifaa vya Tehema mkoani Dodoma.


Vyuo vingine ni Patandi, Tarime, Mpuguso, Sumbawanga, Mpwapwa, Tukuyu , Morogoro na Korogwe.




Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ualimu nchini Augustino Sahili ameiomba serikali kuharakisha kukamilisha mpango wa kuunganisha vyuo vyote vya Ualimu vya umma na Mkongo wa Taifa.
Baadhi ya Wakuu wa Vyuo vya Ualimu wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu Profesa James Mdoe (hayupo pichani) wakati wa ugawaji wa vifaa vya Tehama kwa Vyuo vya Ualimu. Hafla hiyo imefanyikia mkoani Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.