Ijumaa, 15 Machi 2019

KAMATI YA BUNGE YA KUDUMU YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UKARABATI CHUO KIKUU ARDHI



Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza serikali kwa kutoa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 2.5 za Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Chuo Kikuu Ardhi zilizotengwa katika bajeti ya mwaka 2018/19.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakibadilishana mawazo na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Oscar Mukasa (MB) wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Chuo Kikuu Ardhi.
Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Oscar Mukasa(MB) Jijini Dar es Salaam baada ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu hiyo ambayo ni ujenzi wa maabara, ukarabati wa karakana, nyumba za walimu, madarasa na kukamilisha ujenzi wa jengo la Lands.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Suzan Lyimo (MB) wakifuatilia taarifa iliyokuwa ikiwasilishwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Evaristo Liwa (Hayupo pichani) wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Chuo hicho.
Aidha, Mhe. Mukasa pamoja na Kamati wameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kusimamia utekelezaji wa Mradi kwa ubora na weledi mkubwa. Vilevile wamepongeza chuo hicho kwa kutumia vyema wataalamu wake kwenye kutekeleza kazi ya ujenzi.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakipata maelezo ya maendeleo ya ukarabati wa Chuo Kikuu Ardhi kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi.
Katika hatua nyingine Kamati imeshauri Serikali kutoa kipaumbele cha kukiendeleza kituo cha utoaji taarifa za viashiria vya majanga yanayoweza kusababishwa na Volcano na matetemeko ya ardhi katika eneo la Oldonyo Lengai. Aidha wameishauri Serikali kuhakikisha Kituo kinapata vifaa vitakavyokiwezesha kufanya kazi ya kutambua viashiria hivyo katika maeneo yote ya nchi na kutoa taarifa hizo.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakiangalia baadhi ya kazi za mipango miji, usanifu majengo, upimaji na ramani zilizotengenezwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu Ardhi ikiwa sehemu ya mafunzo kwa vitendo.
Awali Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Evaristo Liwa, akitoa taarifa ya utekelezaji kwa Kamati amesema Mradi huo unaogharimu Shilingi Bilioni 2.5 kwa kiasi kikubwa umesimamiwa na wataalamu wa ndani ya Chuo hali ambayo imewezesha kupunguza gharama na ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa wakati .
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Wiliam Ole Nasha akiwaonyesha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii madarasa yanayoendelea kukarabatiwa (Hayapo pichani) wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara katika Chuo Kikuu Ardhi.
Nae Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameishukuru Kamati hiyo kwa kutembelea mradi na ameahidi kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Kamati.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Evaristo Liwa akitoa maelezo ya ndege ndogo isiyo na rubani (Drone) inayotumika kwa ajili ya kuchukua picha anga za maeneo mbalimbali kwa ajili ya kupanga miji, kupima miji, kusaidia wakati wa majanga kama mafuriko na utafiti mbalimbali. Hii ni moja ya jitihada za Chuo Kikuu Ardhi kuboresha teknolojia katika kufundisha na kutatua matatizo katika jamii.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Oscar Mukasa (MB) machapisho ya Chuo Kikuu Ardhi wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni