Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika
kusaidia makundi ya watu wasiojiweza hasa watoto wanaoishi katika mazingira
magumu.
Prof Ndalichako ametoa wito
huo mkoani Kigoma wakati akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya
maombi ya dunia ya umoja wa wanawake wa
kikristo Tanzania CCT na kusema kuwa wanawake wakiamua wana uwezo mkubwa wa kubadili maisha
katika jamii.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa
kilele cha maadhimisho ya siku ya maombi ya dunia kwa wanawake mkoani Kigoma.
Amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele kuyasaidia makundi ya watu wasiojiweza
na hasa watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili wapate haki zao za msingi
hususan elimu.
Amesema wanawake ndio walezi
wa watoto kuanzia ngazi za familia akiwafananisha na walimu kwani wao wana
jukumu la kulea na kufundisha watoto wote.
“Wanawake wenzangu
tukumbushane msemo ambao Mama Salma Kikwete ambae ni mke wa Rais Mstaafu wa
awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewahi kusema kuwa mtoto wa
mwenzio ni wa kwako hivyo tuwasaidie watoto yatima, wa mitaani na wale
wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kutimiza ndoto zao hasa za kupata elimu,” alisisitiza Waziri Ndalichako.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako (aliyepo katikati) akicheza
na moja ya kwaya iliyotumbuiza wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya
maombi ya dunia kwa wanawake katika Kanisa la Anglikan lililopo mkoani Kigoma.
Pia, Waziri Ndalichako
amewataka wanawake nchini kudumisha mshikamano miongoni mwao na kuunga mkono
juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwa vitendo kwa kuhakikisha
wanafanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kwa lengo la kujipatia kipato.
Akiwa mkoani humo waziri
Ndalichako pia aliwatembelea wagonjwa ambao wamelazwa katika hospitali ya rufaa
ya Kigoma Maweni na kutoa misaada
mbalimbali kwa wagonjwa hao.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwajulia hali baadhi
ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kigoma Maweni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.