Jumatano, 22 Mei 2019

WIZARA YA ELIMU YAKUTANA NA UJUMBE TOKA CHINA


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Avemaria Semakafu ameongoza majadiliano kati ya Wizara na Ujumbe kutoka taasisi ya China-Africa Industrial Cooperation Promotion Center ya nchini China yaliyolenga kutambua maeneo ya kushirikiana na nchi hiyo katika Sekta ya Elimu na jinsi ambavyo elimu kupitia teknolojia inaweza kuchangia moja kwa moja kwenye uchumi wa viwanda.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Uongozi wa Wizara na viongozi kutoka taasisi mbalimbali za nchini China ambazo zinajihusisha na masuala mbalimbali ikiwemo Tehama.  Ujumbe huo kutoka China uliongozwa na Mkurugenzi wa taasisi ya China-Africa Industrial Cooperation Promotion Center, Bw. Wenbao Tan.

Katika majadiliano hayo wamekubaliana kuona uwezekano wa kushirikiana katika maeneo ya ufundishaji wa lugha ya Kichina katika vyuo vya ualimu na ufundi, uanzishwaji wa maabara za kufundishia lugha, uboreshaji mifumo ya elimu mtandao pamoja na uanzishwaji wa hospitali ya kujifunzia.
Ujio huo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya maeneo makuu ya ushirikiano wa kimaendeleo kati ya China na Afrika yaliyofikiwa katika mkutano uliofanyika Afrika Kusini mwaka 2015.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni