Balozi
wa Finland Pekka Makka ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa
utekelezaji wa miradi ya Sekta ya Elimu inayofadhiliwa na Finland ambayo
imewezesha uboreshaji katika maeneo mbalimbali ya sekta hiyo.
Balozi
Makka ametoa pongezi hizo jijini Dodoma alipofika ofisi za Wizara na kukutana
na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha kwa lengo la
kushukuru kwa ushirikiano pamoja na kuaga baada ya kumaliza muda wake ambapo amesema
kupitia utekelezaji wa miradi hiyo wameiona sekta ya elimu ikiboreshwa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akisalimiana na Balozi wa Finland Pekka Makka alipofika ofisi za Wizara kwa lengo la kushukuru kwa ushirikiano pamoja na kuaga baada ya kumaliza muda wake.
Makka
amesema Wizara ya elimu imeboresha miundombinu katika shule mbalimbali nchini na
kuweka mazingira mazuri ya wanafunzi kujifunza, huku akipongeza walimu kwa kuboresha
mbinu za ufundishaji.
Balozi
huyo amesema Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uboreshaji wa
sekta ya elimu hususan katika maeneo ya Elimu ya Ufundi, Sayansi, Teknolojia na
Ubunifu ili kupanua wigo wa upatikanaji wa mafunzo nchini.
“Tumeona
maboresho makubwa katika sekta ya elimu, nasi kama wafadhili tumefarijika na
hakika tunaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendelea kuboresha sekta
hii muhimu, na ninaahidi kuwa Balozi anayekuja kunipokea ataendeleza ushirikiano
huu,” amesema Makka.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungumza na Balozi wa Finland Pekka Makka alipofika ofisi za Wizara kwa lengo la kushukuru kwa ushirikiano pamoja na kuaga baada ya kumaliza muda wake ambapo ameipongeza wizara kwa kutekeleza vyema miradi mbalimbali.
Naye
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameishukuru
Finland kwa ufadhili wa Euro milioni 52
kwa ajili ya miradi, ambapo amesema kupitia ufadhili huo Tanzania imeshirikiana
na Finland kuongeza fursa za elimu na mafunzo kwa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo
rasmi kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu
Wazima, hususan kwa kuwajengea uwezo watekelezaji wa mpango wa ‘Intergrated
Post Primary Education (IPPE)’ na mpango wa ‘Intergrated Programme for Out of
School Adolescents (IPOSA)’.
Miradi
mingine aliyoitaja ambayo imefadhiliwa na Finland ni pamoja elimu ya afya na michezo katika vyuo vya
ualimu ambayo ililenga kuwajengea maarifa na ujuzi wakufunzi na walimu tarajali waweze kufundisha shuleni
kwa kuzingatia umuhimu wa michezo shuleni na kwa maendeleo ya taifa, mradi wa
Tehama, (TANZAICT) unaotekelezwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),
mradi ambao umewezesha kuwepo na mifumo ya kukuza ubunifu na kuwezesha mfuko wa
kufadhili wabunifu wadogo.
Aidha,
Naibu Waziri amesema ushirikiano kati ya Wizara na Finland utakaoendelea
unalenga zaidi katika Mafunzo ya Ufundi na Ubunifu na kwamba umekuja kwa wakati
sahihi ambapo nchi inaelekea katika uchumi wa kati kupitia viwanda.
“Ili
kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda
ni lazima tuwe na rasilimaliwatu ya kutosha iliyoelimika na yenye maarifa na
ujuzi kwa ajili ya viwanda na pia itakayoweza kujiajiri,” amesisitiza Ole
Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha, Balozi wa Finland Pekka Makka wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa wizara mara baada ya kikao na Balozi huyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.