Jumapili, 7 Julai 2019

UJENZI WA OFISI ZA UTHIBITI UBORA WA SHULE WAANZA KWA KASI WILAYANI MISUNGWI


·        Naibu Waziri Ole Nasha afanya ziara kukagua asisitiza viwango katika utekelezaji wa mradi huo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza kwa usimamizi mzuri wa mradi wa ujenzi wa ofisi ya uthibiti ubora wa shule wa wilaya hiyo inayojengwa katika kata ya Igokelo kijiji cha Mapilinga mkoani humo.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa pongezi hizo alipofanya ziara katika Wilaya hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi hiyo ambapo amesema ameridhishwa na hatua ambayo ujenzi umefikia huku mkazo ukiwa kuzingatia ubora wa ujenzi wa jengo hilo.

“Kwa kweli mnakwenda vizuri, kama fedha mmepokea mwezi Mei mwaka huu tokea ujenzi uanze michakato yote ni kama mmetumia mwezi mmoja na tayari mmeshapaua ni jambo jema. Lakini niwapongeze zaidi kwa kuwa ujenzi huu miundombinu yake imezingatia watu wenye mahitaji maalum zingatieni ubora wa jengo katika kukamilisha kazi hii,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha
Naibu Waziri wa Elimu, Saysnia na Teknolojia William Ole Nasha akikagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Uthibiti ubora wa shule Wilaya ya Misungwi Jijini Mwanza.
Alisema ujenzi wa Ofisi za Uthibiti ubora wa shule ni mwendelezo wa nia ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuamua kuimarisha Idara ya Uthibiti Ubora wa shule ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa lengo la kuinua ubora wa elimu nchini.

Ole Nasha ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuboresha Sekta ya Elimu kwa kuwa zina lengo la kuimarisha elimu ya watoto wetu lakini pia kutumia fursa zinazokuja na miradi hiyo kujiingizia kipato kwani kwa sasa Serikali imeamua kutumia utaratibu wa Force Akaunti katika utekelezaji wa miradi yake kwani utaratibu huo umeonesha kuwa na mafanikio lakini pia unawanufaisha wananchi walio karibu na mradi unapotekelezwa.

“Wanamisungwi 34 wamefaidika na ujio wa mradi wa ujenzi wa ofisi hii ya Uthibiti ubora wa shule wapo waliopata nafasi ya kufanya kazi za ujenzi na wale wanaofanya bishara ya chakula na vinywaji na hili ndilo lengo la Serikali,’aliongeza Naibu Waziri ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipata maelezo ya namna mradi wa ujenzi wa ofisi ya uthibiti ubora wa shule wilaya ya Misungwi unavyotekelezwa kutoka kwa Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule wa Wilaya ya Misungwi Faustin Salala.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa Ofisi hiyo Mthibiti Mkuu wa ubora wa Shule Wilaya ya Misungwi Faustini Salala alisema ujenzi wa ofisi hizo umeanza mwishoni mwa mwezi Mei 2019 na unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti, 2019 na utatumia zaidi ya shilingi milioni 150.

Mradi wa Ujenzi wa ofisi ya Uthibiti Ubora wa shule katika wilaya ya Misungwi ni moja  ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa ofisi 100 za aina hiyo zinazojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchi nzima ili kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watendaji wa Idara hiyo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na baadhi ya Walimu pamoja na wananchi mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za Uthibiti ubora Wilaya ya Misungwi. Amewataka kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu kwani inalenga kuboresha elimu ya watoto wetu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.