Naibu Waziri Ole Nasha amesema hayo mkoani Geita wakati wa ziara ya
kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya Elimu inayotekelezwa mkoani humo,
ambapo amesema serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayehujumu ama kutumia
vibaya fedha hizo zilizotolewa na wizara kwa ajili ya kujenga ofisi hizo.
Amesema miradi ya ujenzi wa ofisi hizo ni muhimu sana kwa wizara kwani
ili kuwa na maendeleo katika sekta ya elimu lazima kuwa na uthibiti ubora wa
shule ulio mahiri, wenye uwezo wa kukagua shule na wenye vitendea kazi vya
kuwezesha wathibiti ubora wa shule kufanya kazi katika mazingira wezeshi.
“Kama tunataka kuwa na maendeleo katika sekta ya Elimu lazima kuwe na
usimamizi thabiti na ndio maana tumechukua hatua mbalimbali kuhakikisha
tumeboresha idara ya uthibiti ubora kwa kuhuisha mfumo kutoka kuwa ukaguzi na
kuwa uthibiti kwa maana kwamba unashirikisha kila mtu katika hatua zote,”
amesema Ole Nasha.
Ole Nasha amesisitiza kuwa haiwezekani kufanya kazi ya uthibiti ubora wa
shule kama hakuna ofisi, vitendea kazi ikiwemo magari na ndio maana kila Afisa
Elimu wa Kata kwa nchini nzima alipewa pikipiki ya kumwezesha kufanya kazi.
Serikali pia ilitoa magari 45 kwa wilaya mbalimbali na sasa halmashauri
zipatazo 100 zinajengewa ofisi za uthibiti ubora.
Naibu Waziri Ole Nasha amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa ofisi
hizo, Wizara itapeleka vifaa vyote muhimu kwenye ofisi hizo ili kurahisisha
kuchakata taarifa zote za elimu kutoka maeneo yote ya nchini kwa lengo la
kurahisha huduma za kielimu.
Aidha, Waziri Ole Nasha amesema ameridhishwa na usimamizi na matumizi ya
fedha za ujenzi wa ofisi za uthibiti ubora Kanda ya Ziwa ambayo inajumuisha
Mikoa ya Geita, Mwanza na Mara ambayo kwa ujumla inajengewa ofisi 15 zenye
thamani zaidi ya bilioni 2.28.
Katika ziara hiyo Waziri Ole Nasha amekagua majengo ya uthibiti ubora wa
shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Halmashauri ya mji wa Geita. Ole
Nasha pia amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni mawili na vyoo katika
shule ya sekondari Mwatulole ambayo inatarajiwa kuanzisha kidato cha tano hivi
karibuni.
Shule nyingine aliyotembelea ni shule ya sekondari ya Wasichana
Nyankumbu ambapo ametembelea chumba cha kompyuta na ameahidi kupeleka kompyuta
50 shuleni hapo ili kuongeza ari ya kujifunza.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ali Kidwaka
alimweleza Naibu Waziri kuwa ameshirikiana na watendaji wengine kufanikisha
ujenzi ambao uko kwenye hatua ya ukamilishaji na kuahidi kuwa ataendelea
kusimamia ili jengo hilo likamilike kwa wakati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.