Wakati Mradi wa ujenzi wa
Chuo cha Ualimu Kabanga kilichopo Wilayani Kasulu mkoani Kigoma ukiendelea kwa kusuasua Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ametoa siku 15 kwa
Mshauri Elekezi BICO kupitia upya
gharama za ujenzi wa mradi huo ambazo ni
zaidi ya shilingi bilioni kumi
ili kujiridhisha kama fedha hiyo inaendana na ukubwa wa mradi.
Prof. Ndalichako ametoa
agizo hilo mara baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo ambapo pamoja na
kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi ametilia shaka gharama ya ujenzi ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni
kumi kutumika ndivyo sivyo kutokana na aina ya majengo yanayojengwa katika chuo
hicho kuwa ya thamani ndogo.
"Hivi ni vighorofa
mtoto na narudia ni vighorofa mtoto huwezi kuniambia kwamba majengo haya ambayo
kwanza ni machache, pili siyo ghorofa zile kubwa kama tulizojenga katika miradi
mingine tena kwa gharama ndogo ya shilingi bilioni sita zinazidiwa na vighorofa
hivi hapa kuna kitu hakipo sawa nataka ndani ya siku kumi na tano gharama za
mradi zipitiwe upya kwa kila jengo na nipewe taarifa vinginevyo mratibu wa
miradi hii utafute kazi nyingine," alisema Prof. Ndalichako.
Injinia wa mradi wa ujenzi
wa Chuo cha Ualimu Kabanga akimuonesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof Joyce Ndalichako namna chuo cha Ualimu Kabanga kitakavyoonekana baada ya
ujenzi kukamilika
Kuhusu kusuasua kwa Mradi
Waziri Ndalichako amemtaka Mkandarasi huyo ambaye ni Kampuni ya SUMA JKT
kuongeza kasi ya kufanya kazi akisisitiza ziletwe mashine za kisasa ambazo
zitarahisisha kazi pamoja na kuongeza vibarua kwenye eneo la kazi.
"Huwezi kutekeleza
mradi wa zaidi ya shilingi bilioni kumi kama nyumba yako unayojenga, yaani una
kamashine kamoja tena kakusukuma,vibarua wenyewe inaonekana umewaleta leo baada
ya kusikia nakuja kukagua, hii haikubaliki tunataka kazi ifanyike usiku na
mchana kwa sababu pesa zipo lazima mradi ukamilike haraka," alisema
Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu,
Kabanga unaojengwa na Wizara kupitia Mradi wa TESP wilayani Kasulu mkoani Kigoma
Mapema akitoa taarifa
ya mradi huo, Kaimu Mkuu wa Kanda ya Ujenzi SUMA JKT, Luteni Kanali
Onesmo Njau amesema mpaka sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia thelathini na
kudai kukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo
usumbufu wa kupata vifaa vya ujenzi kama saruji na mchanga.
"Mheshimiwa Waziri
tulikuwa tukitegemea kupata saruji kwa kampuni ya Dangote lakini kwa sasa
inabidi tufuate wenyewe Dodoma na hivyo kutumia muda mwingi kusubiri vifaa
vifike kwenye eneo la mradi," alisema Kanali Njau.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga
Kasulu Mkoani Kigoma
Naye mshauri elekezi wa
mradi huo kutoka BICO, Fred Munishi amekiri kuwa kazi inasuasua na kusema kuwa
tayari ametoa maelekezo kwa Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi taarifa ambayo
hata hivyo imeonekana kukinzana na taarifa ya Mkandarasi na hivyo kutakiwa
kufanya kazi kwa karibu na Mkandarasi.
"Inaonekana hapa hakuna
maelewano mazuri baina ya Mkandarasi na mshauri elekezi, sitaki mivutano kazini
kaeni pamoja fanyeni kazi ya serikali na mkiendelea hivi tutawaondoa,"
alisema Waziri Ndalichako.
Akiwa katika Halmashauri ya
wilaya ya Kasulu, Waziri Ndalichako pia amekagua miradi mingine minne ya elimu
katika shule za sekondari na msingi za Kigodya, Ruhita, Nyantare na Kasyenene na kueleza kuridhishwa na kazi
huku akisisitiza kuwa serikali inatoa fedha ili kuona matokeo.
Katika ziara hiyo Waziri
Ndalichako aliambatana pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Dkt. AveMaria
Semakafu pamoja na Mratibu wa Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo pamoja na ule
wa TESP.
Muonekano
wa sasa wa hatua ya ujenzi wa baadhi ya majengo katika eneo la mradi wa Chuo
cha Ualimu Kabanga wilani Kasulu Mkoani Kigoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.