Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako ametilia shaka matumizi ya fedha za serikali
zaidi ya shilingi milioni mia tano zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi na
ukarabati wa shule ya sekondari Kasangezi iliyopo wilayani Kasulu mkoani
Kigoma.
Akizungumza mara baada ya
kukagua utekelezaji wa mradi huo waziri Ndalichako amesema shule hiyo imepatiwa
zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 4,
mabweni 4 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 katika kila moja, matundu ya
vyoo 10, bwalo pamoja na ukarabati wa maabara.
Ndalichako amesema kazi iliyofanyika haiendani na fedha
iliyotolewa kutokana na miundombinu hiyo kujengwa chini ya Kiwango.
“Milango ya madarasa na hata
ya mabweni mmetengeneza kwa mbao laini tofauti na BOQ pamoja na kuwa laini ina
uwazi hii nataka itolewe, tazama sakafu imeshaharibika hapa hata mwaka
haujaisha mabweni mliambiwa ya watu themanini mmejenga ya watu sitini"
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiangalia mlango wa
darasa ambao umetengenezwa kwa mbao laini kinyume cha taratibu katika shule ya
sekondari Kasangezi
Kufuatia hali hiyo ndalichako
ameagiza kuwa ujenzi wa mabweni urudiwe kwa kuzingatia BoQ na ameaguza ujenzi
huo uwe umekamilika ifikapo desemba.
"Nitakuja mwenyewe
mwezi wa kwanza kukagua kama hayo yatakuwa hayajatekelezwa mengine yatafuata,”
amesema waziri Ndalichako.
Aidha waziri Ndalichako
amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya kumuondoa
mara moja shuleni hapo mkuu wa shule hiyo kwa kushindwa kusimamia vizuri kazi hiyo na hivyo kuisababishia
hasara serikali.
“Kwanza ujenzi wa mara ya
kwanza hata matofali hukununua ulichukua kwenye benki ya wananchi na tayari
nilikuwa nimeleta fedha sasa kwanini hukujiongeza hata ukarekebisha ofisi ya
Mkuu wa Shule ambayo iko katika hali isiyoridhisha vitu vingine ni kudhalilisha
Serikali, Mkurugenzi muahamishe huyu katika shule hii,” alisema waziri
Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akikagua maendeleo ya ujenzi wa moja ya bweni katika shule ya
sekondari Kasangezi iliyoko Halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Waziri Ndalichako pia
ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kasulu
kufuatilia muenendo wa upatikanaji wa madawati miamoja themanini
yaliyonunuliwa katika mradi huo kama yametimia na yamenunuliwa kwa kufuata
utaratibu.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Kasulu Kanali Saimon Anange amekiri kuwepo uzembe katika kusimamia
miradi hiyo na kumuhakikishia waziri Ndalichako kuwa ofisi yake itafanyia kazi
maelekezo yote aliyoyatoa katika ziara hiyo.
Waziri wa Elimu Sayansi na
Teknolijia Prof. Joyce Ndalichako yupo mkoani Kigoma Kwa ziara ya Kikazi
akikagua miradi ya elimu inatekelezwa kupitia fedha za Programu ya lipa kwa
matokeo EP4R.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua mlago wa darasa ambao umetumia mbao laini tofauti na maelekezo katika shule ya sekondari Kasangezi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.