Alhamisi, 6 Februari 2020

MAKISATU 2020 KUENDELEA KUIBUA WABUNIFU

Serikali imesema inatambua umuhimu na mchango wa ubunifu na teknolojia katika kurahisisha na kuongeza ufanisi  katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu kuanza kwa Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) 2020, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema  mashindano hayo ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu na ugunduzi unaofanywa na watanzania.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano mara baada ya kuzungumza na Waandishi wa habari jijini Dodoma.  Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Leonard Akwilapo na kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Sylvia Lupembe.

"Lengo kubwa la MAKISATU pamoja na kukuza na kusaidia kubiasharisha, yanatoa fursa kwa wabunifu na wagunduzi wa teknolojia mbalimbali kujitangaza na kutangaza kwa wadau ubunifu unaozalishwa," amesisitiza Ole Nasha.
Mwakilishi wa Benki ya CRDB, Prosper Nambaya akizungumza wakati wa Mkutano wa Waandishi wa habari kuzungumzia kuanza kwa mashindano ya MAKISATU, 2020 jijini Dodoma.
Ole Nasha amesema MAKISATU inawalenga wabunifu kutoka makundi ya shule za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi stadi, vyuo vya kati, vyuo vikuu, Taasisi za utafiti na Mfumo usio rasmi.

Baadhi ya washiriki waliohudhuria Mkutano wa kuzungumzia kuanza kwa Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknonojia na Ubunifu (MAKISATU) 2020 jijini Dodoma, wakimsikiza Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (hayupo pichani) wakati akizungumza na Waandishi wa habari.

Aliongeza kuwa kupitia MAKISATU 2019 Serikali imewaibua na kuwatambua wabunifu wachanga zaidi ya 415 huku wabunifu 60 mahiri wakiendelezwa ili ubunifu wao ufikie hatua ya kubiasharishwa.


Kiongozi huyo ametoa wito kwa watanzania wenye ubunifu mbalimbali kushiriki katika mashindani hayo na amewashukuru Benki ya CRDB kwa kukubali kufadhili mashindano hayo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Wateja Wakubwa kutoka CRDB, Prosper Nambaya amesema Benki hiyo imeamua kuwa na ushirikiano endelevu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kusaidia kukuza ubunifu unaozalishwa nchini kutokana na kuwepo kwa watu wengi wenye mawazo ya kibunifu yanayopaswa kuendelezwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni