Alhamisi, 6 Februari 2020

SERIKALI KUJENGA SHULE ZA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM KILA MKOA

Serikali imesema itaendelea na mpango mkakati wa kutekeleza elimu bila malipo pamoja na kutoa vipaumbele kwa watu wenye ulemavu kupata elimu iliyo bora.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu wakati wa ufungaji wa mafunzo ya TEHAMA na Teknolojia Saidizi kwa wakufunzi na walimu wa Sekondari wenye mahitaji maalum.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu akiongea wakati wa ufungaji wa mafunzo ya Tehama na Teknolojia Saidizi kwa Wakufunzi na Walimu wa Sekondari wenye mahitaji maalumu jijini Dar es Salaam.
Dk. Semakafu amesema  serikali imejipanga kuhakikisha walimu  na wanafunzi wanapata elimu ya Tehama, elimu jumuishi sambamba na kujenga shule zao maalum katika kila mkoa ambapo kwa sasa wameanza na mkoa wa Katavi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu akitoa maelekezo kwa mmoja wa washiriki wa mafunzo ya Tehama na Teknolojia Saidizi OUT, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo awali ilielezwa kuwa tayari serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 5.9 kwa ajili ya kununua na kusambaza vifaa maalum vya kielimu saidizi katika shule za msingi na sekondari zinazopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini.

“Hii kazi pia si ndogo, napenda kwa namna ya kipekee kabisa kutumia nafasi hii kuushukuru Uongozi wa Chuo Kikuu Huria kwa kukubali kuendesha mafunzo haya hapa chuoni na kutoa wawezeshaji, vifaa pamoja na miundombinu mingine kwa ajili ya kufanikisha mafunzo haya muhimu,’’ amesema Dk. Semakafu.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya Tehama na Teknolojia Saidizi akiwa katika mafunzo yaliyofanyika Chuo Kikuu Huria jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu.
Aliongeza kuwa mafunzo waliyoyapata ni muhimu kwani yatawasaidia katika matumizi ya TEHAMA kwenye  ufundishaji na ujifunzaji, kutafuta rejea mbalimbali za kielektroniki kwenye mitandao na kutumia teknolojia saidizi zinazowezesha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Mwalimu wa shule ya sekondari ya Binti Mussa iliyopo Kiwalani jijini Dar es Salaam, Anna Mbogo alisema wanaishukuru kwa  dhati  Wizara ya Elimu kwa kuona umuhimu wa kutoa  mafunzo kwa walimu wenye mahitaji maalum.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Tehama na Teknolojia Saidizi kwa Wakufunzi na Walimu wa sekondari wenye mahitaji maalumu wakifuatilia hotuba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu (hayupo pichani)  wakati wa kufunga mafunzo hayo jijini Dar es Salaam.
“Mafunzo haya  yalilenga kutujengea uwezo sisi walimu kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya sasa, pia tunaushukuru uongozi wa OUT chini ya serikali ya awamu ya tano kuonesha bayana nia ya kuwasaidia walimu wenye mahitaji maalum na kuwathamini watu wenye ulemavu kwa kuajiri watu wenye ulemavu,’’ amesema Mwalimu Anna.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.