Ijumaa, 24 Novemba 2017

Dkt. Akwilapo awataka wahitimu wa ADEM kusimamia kanuni na taratibu katika utendaji kazi.

 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leornard Akwilapo amewataka wahitimu wa kozi za Uongozi na Usimamizi wa Elimu zinazotolewa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka(2014), Sheria, Kanuni na Taratibu za Elimu ili kupunguza migogoro shuleni

Katibu Mkuu ameyasema hayo katika mahafali ya Ishirini na tano (25) yaliyofanyika katika Chuo hicho kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo amewataka ADEM  kuendelea kusimamia utekelezaji wa Mtaala kwa ufanisi, kutoa takwimu sahihi za shule, kupanga mipango ya maendeleo ya shule inayotekelezeka, kusimamia fedha za elimu bila malipo kwa ufanisi.

Eneo lingine ambalo Katibu Mkuu ametaka litiliwe mkazo ni    pamoja na kudhibiti nidhamu za wanafunzi mara warudipo katika vituo vyao vya kazi.

Dkt. Akwilapo amesema mafunzo ya uongozi na usimamizi wa Elimu pamoja na Ukaguzi wa Shule ni muhimu katika kuwapa uwezo walimu na viongozi wa elimu kufanya kazi zao kwa weledi, ufanisi na kwa kujiamini zaidi hususani katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.

Amewataka wahitimu kuwa chachu ya mabadiliko katika Uongozi na Utawala Bora pamoja na  Uthibiti Ubora wa Shule nchini kwa kutumia ujuzi, maarifa, stadi na mbinu mpya walizozipata katika mafunzo ikiwa ni pamoja na   maarifa waliyoyapata kuyaeneza kwa walimu ambao hawajapata fursa ya kupata mafunzo hayo.





Chuo Kikuu Ardhi chaadhimisha miaka 10

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa kassim Majaliwa amekitaka Chuo Kikuu cha Ardhi nchini kuendelea kutekeleza mpango mkakati waliojiwekea ili kufikia malengo yanayo kusudiwa na Taifa.

Waziri Mkuu  Majaliwa ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya chuo hicho ambapo amekitaka , Chuo hicho kuwa na kamapuni itakayosimamia ujenzi katika maeneo mbalimbali hapa nchini na siyo jina la Chuo kutumika vibaya na kuratibu sifa ya Chuo.
Waziri Majaliwa amesema  Chuo hicho kimekuwa kikiisaidia serikali kujenga majengo yenye viwango kwa garama nafuu, hivyo amezitaka taasisi za serikali kukitumia Chuo hicho katika ujenzi wa majengo mbalimbali.

 Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Chuo kikuu cha Ardhi kimekuwa kikifanya vizuri katika ujenzi, usanifu wa majengo na kwa kutambua kazi ya Chuo hicho  tayari Wizara imetoa zaidi ya bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya Ualimu, na shule.
Baada ya kukamilika kwa mkutano huo, Waziri Ndalichako alikutana na wanafunzi wa Chuo hicho kwa ajili ya kusikiliza changamoto mbalimbali ambapo wanafunzi walimweleza Waziri kuwa hadi sasa hawajaingiziwa mikopo yao kwa kile kilichoelezwa kuwa wanafunzi bado hawajafungua Akaunti, na ndiyo Wizara alipohitaji maelezo kutoka kwa Afisa mikopo majibu ambayo waziri hakuridhika nayo na ndiyo alipoomba maelezo.

Hata hivyo kutokana na maelezo ambayo hakuridhika nayo,Waziri aliamua kuondolewa mara moja kwa afisa mikopo katika Chuo hicho.


Jumanne, 21 Novemba 2017

China na Tanzania kuendelea kushirikiana katika Sekta ya Elimu

Jamhuri ya Watu wa China imesema itaendela kuisaidia Tanzania katika sekta ya Elimu kwenye eneo la Elimu ya Juu, utoaji wa mafunzo ya Ufundi pamoja na kusaidia garama za uchapishaji wa vitabu vya masomo ya Sayansi kwa ajili ya shule za  msingi na Sekondari.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Jamuhuri ya watu wa China nchini Tanzania Wang Ke wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Profesa Joyce Ndalichako katika ofisi ndogo zilizopo jijini Dar es Saalam.

Katika mazungumzo yao Waziri Ndalichako amesema garama za uchapaji wa Vitabu ni kubwa hivyo ni vyema Wizara ikawa na mitambo yake ya kuchapia vitabu ambayo itakuwa endelevu suala ambalo Balozi Wang Ke  amekubaliana nalo na kuitaka Wizara kuandaa maombi ya mashine hiyo ili ubalozi uweze kufanyia kazi.


Jumatatu, 20 Novemba 2017

Waziri Ndalichako: Ili shule isajiliwe lazima ikidhi vigezo

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema ili shule isajiliwe lazima iwe imekidhi vigezo ikiwa ni pamoja na kuwa na madarasa ya kutosha, nyumba za walimu, ofisi za walimu, matundu ya vyoo, pamoja na maabara endapo shule itakuwa ni ya Sekondari.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa halmashauri ya Mbulu iliyopo mkoani Manyara ambapo amesema ni kweli serikali inahitaji ziwepo shule nyingi ambazo zinavigezo, siyo kuwa na shule ambazo hazina vigezo.

"Shule za nyasi katika Serikali hii ya awamu ya tano zitabaki kuwa historia kwa kuwa serikali inajenga na kuboresha miundombinu ya kujifunzia na ile ya kufundishia, sasa ili shule isajiliwe lazima iwe imekidhi vigezo siyo bora shule bali tunahitaji shule zilizobora na zenye viwango vinavyokubalika" amesema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema   kazi ya usajili ni nyepesi sana ambayo haichukui muda mrefu endapo vigezo vinakuwa vimetimia,  lakini kazi kubwa ni kuhakikisha miundombinu bora inayokubalika inakuwepo ili shule iweze kusajiliwa.

 Hivyo amewasihi wadau wote wa Elimu kuhakikisha shule zinapojengwa zinazingatia na kukidhi  vigezo kabla ya kusajiliwa.



Alhamisi, 16 Novemba 2017

Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii yakagua Shule ya Ihumwa

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya huduma za maendeleo ya jamii imepongeza juhudi zinazofanywa na Wizara ya Elimu, Sanyasi na Teknolojia kwa kushirikiana na OR TAMISEMI katika kuboresha miundombinu ya shule, ikiwa ni pamoja na kusimamia fedha zinazotengwa kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Peter Serukamba wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa 9, matundu ya vyoo na jengo la Utawala katika shule ya msingi Ihumwa ujenzi ambao umetekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia programu ya Lipa kulingana na Matokeo, yaani P4R.
Ziara hiyo imejionea madarasa mapya 9, ukarabati wa vyumba vya madarasa 11, Jengo la utawala na ujenzi wa vyoo ambavyo vyoye vimegharimu milioni 168.

Mwenyekiti wa kamati hiyo pia amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu kutoa fedha kwa ajili ya kuchimba kisima katika shule ili kuondoa adha ya upatikanaji wa maji katika shule hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amemhakikishia Mwenyekiti wa kamati hiyo kuwa Wizara imepokea maelekezo na kuahidi kuyafanyia kazi.