Waziri Ndalichako amesema hayo leo mkoani Morogoro wakati wa Kikao kazi kilichohusisha Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake cha kujadili na kujengeana uwezo kuhusu namna bora ya kubaini na kukabiliana na viashiria hatarishi katika maeneo ya kazi.(Risk Identification and Risk Managment).
Waziri Ndalichako amesema kupitia kikao kazi hicho watendaji wataweza kujifunza na kubaini mapema viashiria ambavyo vitaonekana kukwamisha utekelezaji wa mipango ya wizara.
"lengo hapa ni kuzuia madhara badala ya kusubiri madhara yatokee, hivyo kupitia kikao kazi hiki watendaji watajifunza kwa lengo la kuzuia na kutekeleza malengo ya Wizara kama yalivyokusudiwa,"amesema Waziri Ndalichako
Waziri Ndalichako pia amezitaka Taasisi na Watendaji wa Wizara hiyo kuanzia leo kuacha mara moja kulipana stahili ambazo hazifuati miongozo na nyaraka za serikali.
Profesa Ndalichako ametaja baadhi ya stahili ambazo zimekuwa zikilipwa bila kufuata taratibu na miongozo hiyo kuwa ni pamoja na posho za kujikimu, Nyumba, umeme na simu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amesema mkutano huo umelenga kuondoa viashiria hatarishi ambavyo vimekuwa vikikwamisha ufanisi katika utendaji kazi wa wizara na kuwataka washiriki wa mkutano huo kuandaa mpango mkakati wa kuweza kutambua mapema viashiria hatarishi na kuvifanyia kazi ili kufikia malengo ya wizara.
Kikao kazi hicho ambacho kimeanza leo kitahusisha pia Wakurugenzi wasaidizi, waratibu wa miradi na wasaidizi wa miradi, wathibiti ubora wa shule kanda, wakuu wa vyuo vya Elimu ya Ualimu, na watumishi kutoka kila Idara wa wizara hiyo.