Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha amesema Serikali
haitafumbia macho vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanafunzi na kuwa Sheria
kali zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa
kauli hiyo leo Mkoani Dodoma wakati wa mahojiano maalumu na Shirika la
Utabgazaji la Taifa - TBC ambapo amesema Sheria za nchi ziko wazi kwa mtu
yeyote atakaebainika kufanya vitendo vya ngoni basi adhabu yake ni miaka 15
jela hadi kifungo cha maisha.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha akifanya
mahojiano na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania-TBC wakati huu ambapo
Mataifa mbalimbali yakijielekeza katika kudhimisha siku ya mtoto wa Afrika. Mahojiano
hayo yamefanyika Jijini Dodoma ambapo Naibu Waziri ameelezea pia mafanikio
mbalimbali kuhusu sekta ya Elimu.
Mheshimiwa Ole Nasha pia ameitaka
Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule nchini kuhakikisha unafanya ufuatiliaji kwa
lengo la kuhakikisha Elimu bora inapatikana nchini kwa kuwa hilo ndiyo jukumu lao.
“Kuna maeneo bado Idara ya
uthibiti ubora haijafanya vizuri, mfano katika hili tukio la St. Florence Idara
hiyo ina kitu cha kujibu,” licha ya kuwa vyombo vingine vya Sheria vinaendelea
na uchunguzi lakini na sisi ndani ya Wizara tunafanya uchunguzi kuona nani kazembea
katika suala hilo,” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri pia amewataka wazazi
kuhakikisha watoto wote waliofika umri wa kwenda shule wanakwenda shule kwa
kuwa hivi sasa Elimu msingi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha Nne
inatolewa bure.
Akizungumzia kuhusu viwanda
Mheshimiwa Ole Nasha amesema vyuo vya ufundi ndiyo njia sahihi ya kulipeleka
Taifa katika Uchumi wa Kati, hivyo kupitia vyuo hivyo Taifa litapata
nguvukazi na sahihi ambayo itatumika kwenye viwanda.