Dkt. Semakafu amesema hayo leo mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya Force Akaunti ambao ni utaratibu unaotumika kwenye ujenzi au ukarabati kwa kutumia malighafi za ujenzi na mafundi waliopo eneo husika.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akizungumza wakati akifungua mafunzo ya
matumizi ya Force Akaunti yanayofanyika mkoani Morogoro ambapo amewataka
washiriki wa mafunzo kuwa wazalendo wanaposimamia miradi ya ujenzi
inayotekelezwa na Serikali.
Dkt. Semakafu amesema Force Akaunti ikitumika vizuri
inaonyesha thamani ya Fedha lakini pia utaratibu huo hauna mabadiliko ya
gharama wakati wa kutekeleza ujenzi au ukarabati tofauti na kutumia mkandarasi
katika kutekeleza miradi ya Serikali.
“Force Akaunti ipo kisheria na kinachohitajika ni uzalendo, pia fedha inayotengwa kwa ajili ya ujenzi haiguswi na kuwa hii inatakiwa ioneshe thamani ya Fedha kwa maana matokeo makubwa kwa fedha kidogo,” alisisitiza Dkt. Semakafu.
Washiriki wa mafunzo wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakurugenzi na Wakurugenzi wasaidizi wa VETA, Maafisa VETA wakifuatilia mafunzo ya Force Akaunti.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt. Noel Mbonde amezitaka Mamlaka za Ufundi Stadi VETA kuhakikisha zinaleta mabadiliko ili nchi iweze kufikia malengo ya uchumi wa viwanda.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanaratibiwa na mradi wa kukuza Maarifa, Stadi na ujuzi (ESPJ) yanahusisha Wakurugenzi wa halmashauri za Kasulu,Ngorongoro,Kongwa,Nyasa, Wakurugenzi wa Kanda VETA, Wakurugenzi wasaidizi kutoka Makao Makuu VETA, Maafisa kutoka VETA.
Picha ikimuonesha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu baada ya kuwasili katika ukumbi wa mkutano mkoani Morogoro akiwa ameongozana na Mkurugenzi wa Ufundi na mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt. Noel Mbonde, na mratibu wa mradi wa kukuza Maarifa, stadi na Ujuzi (ESPJ) Dkt. Keneth Hosea