Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia William Ole Nasha ametoa wiki moja kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
Dkt. Leonard Akwilapo kuitisha kikao cha pamoja na Wakala wa Majengo ya
Serikali nchini (TBA) ili kujadiliana kwa pamoja kuhusu changamoto za
utekelezaji wa miradi ya Wizara hiyo inayotekelezwa na TBA.
Naibu waziri ametoa agizo hilo
akiwa Mkoani Ruvuma wakati wa kukagua miundombinu katika shule ya Sekondari
wasichana Songea ambapo amesema Wizara hairidhishwi na kasi ya utekelezaji wa
miradi hiyo hivyo kikao kitakachoitishwa kijielekeze kuona namna bora ya
kukamilisha miradi hiyo au ikiwezekana kuvunja mkataba na wakala huyo.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua miundombinu
katika Shule ya Sekondari ya Wasichana
Songea iliyoko wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.
Ole Nasha amesisitiza kuwa
kuchelewa kwa miradi hiyo kunaiongezea gharama zaidi Serikali lakini pia
hakutatui changamoto iliyokuwa imekusudiwa.
"Wanafunzi wanapata tabu ya
kusongamana wakati tayari Serikali imeliona hilo na kutoa fedha kwa ajili
ya kuboresha miundombinu hiyo ili waweze kusoma ninyi leo
mnaichelewesha sio sahihi,” alisisitiza Naibu waziri Ole Nasha.
TBA walikabidhiwa mradi wa
kukarabati Miundombinu ya shule ya sekondari ya wasichana Songea Machi
2017 na ulitakiwa kukamilika Septemba 2017 ambapo mpaka leo mradi huo
haujakamilika na tayari Wizara imekwishawalipa TBA shilingi
milioni 580 kwa ajili ya kazi hiyo.
Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiongea na walimu wa Shule ya
Sekondari ya Wasichana Songea mara baada ya kukagua miundombinu ya shule hiyo
iliyofanyiwa ukarabati na Wizara. Amewataka walimu kutekeleza majukumu yao kwa
weledi lakini pia kuunga mkono juhudi za Serikali inazozifanya katika kuboresha
miundombinu ya Shule.
Kwa upande wake mwakilishi wa TBA
mkoani Ruvuma mhandisi Matapuli Juma amekiri kuwapo kwa ucheleweshwaji
wa kukamilisha kazi hizo na kuwa kwa sasa wamejipanga kuhakikisha kazi
hiyo inakamilika mapema.
Naibu Waziri Ole Nasha
amekamilisha ziara yake leo mkoani Ruvuma ambapo pia ametembelea Chuo cha
Ualimu Songea na kuongea na walimu pamoja na wanafunzi ambapo amewaeleza kuwa
serikali inatambua changamoto zilizopo katika sekta ya Elimu na imekuwa
ikizishughulikia kila siku ili kuhakikisha Elimu inatolewa katika mazingira
mazuri.
Naibu
Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiongea na wakufunzi wanaofundisha somo la Fizikia katika Maabara ya somo hilo wakati alipotembelea
Chuo cha Ualimu Songea Kilichopo Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma