Jumanne, 2 Oktoba 2018

OLE NASHA AAGIZA KUFANYIKA KIKAO NA TBA KUHUSU UCHELEWESHWAJI WA MIRADI YA WIZARA ELIMU


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ametoa wiki moja kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo kuitisha kikao cha pamoja na Wakala wa Majengo ya Serikali nchini (TBA) ili kujadiliana kwa pamoja kuhusu changamoto za utekelezaji wa miradi ya Wizara hiyo inayotekelezwa na TBA.

Naibu waziri ametoa agizo hilo akiwa Mkoani Ruvuma wakati wa kukagua miundombinu katika shule ya Sekondari wasichana Songea ambapo amesema Wizara hairidhishwi na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo hivyo kikao kitakachoitishwa kijielekeze kuona namna bora ya kukamilisha miradi hiyo au ikiwezekana kuvunja mkataba na wakala huyo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua miundombinu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana  Songea iliyoko wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.

Ole Nasha amesisitiza  kuwa kuchelewa kwa miradi hiyo kunaiongezea gharama zaidi Serikali lakini pia hakutatui changamoto iliyokuwa imekusudiwa.

"Wanafunzi wanapata tabu ya kusongamana wakati tayari Serikali imeliona hilo na kutoa  fedha kwa ajili ya kuboresha  miundombinu hiyo ili waweze kusoma  ninyi leo mnaichelewesha sio sahihi,” alisisitiza Naibu waziri Ole Nasha.

TBA walikabidhiwa mradi wa kukarabati Miundombinu ya shule ya sekondari ya wasichana  Songea Machi 2017  na ulitakiwa kukamilika Septemba 2017  ambapo mpaka leo mradi huo haujakamilika na tayari Wizara imekwishawalipa    TBA shilingi milioni 580 kwa ajili  ya kazi hiyo.  

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiongea na walimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Songea mara baada ya kukagua miundombinu ya shule hiyo iliyofanyiwa ukarabati na Wizara. Amewataka walimu kutekeleza majukumu yao kwa weledi lakini pia kuunga mkono juhudi za Serikali inazozifanya katika kuboresha miundombinu ya Shule. 
Kwa upande wake mwakilishi wa TBA mkoani Ruvuma mhandisi Matapuli Juma amekiri kuwapo kwa ucheleweshwaji wa kukamilisha kazi hizo na  kuwa kwa sasa wamejipanga kuhakikisha kazi hiyo inakamilika mapema. 

Naibu Waziri Ole Nasha amekamilisha ziara yake leo mkoani Ruvuma ambapo pia ametembelea Chuo cha Ualimu Songea na kuongea na walimu pamoja na wanafunzi ambapo amewaeleza kuwa serikali inatambua changamoto zilizopo katika sekta ya Elimu na imekuwa ikizishughulikia kila siku ili kuhakikisha Elimu inatolewa katika mazingira mazuri.


Naibu Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiongea na wakufunzi wanaofundisha somo la Fizikia katika Maabara ya somo hilo wakati alipotembelea Chuo cha Ualimu Songea Kilichopo Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.