Jumamosi, 9 Machi 2019

WIZARA YA ELIMU YAGAWA KOMPYUTA 300 KWA VYUO VYA ELIMU VYA UMMA


Kiasi Cha Shilingi bilioni 1.2 kimetumika  kununulia vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya vyuo vya ualimu vya umma  18, kwa  lengo la   kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji katika vyuo hivyo ili  kuzalisha walimu bora  na wanaoendana na ulimwengu wa Teknolojia.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu Profesa James Mdoe kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati wa halfa ya utoaji vifaa mbalimbali vya TEHAMA zikiwemo Kompyuta 300, UPS 300 na Projector 100 kwa ajili  vyuo hivyo vya Ualimu.

Kaimu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe akigawa vifaa vya Tehama kwa Wakuu wa Vyuo vya Ualimu vya Umma nchini kwa lengo la kuboresha elimu ya Ualimu, hafla hiyo imefanyikia mkoani Dodoma.

Katika hotuba yake, Profesa Mdoe amesema serikali ya Tanzania inawashukuru  washiriki wa maendeleo ambao ni serikali ya CANADA kwa kufadhili mradi wa kuendeleza na kuboresha Elimu ya Ualimu  (TESP ) kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Profesa Mdoe pia amewaasa Wakuu wa Vyuo kutumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyo kusudiwa na ametoa onyo kwa Wakuu wa vyuo wote wanauhujumu jitihada za serikali za kuboresha miundombinu ya vyuo vya Ualimu kuacha mara moja tabia hiyo na kuwataka watumishi wote  kutanguliza maslahi ya Taifa ikiwa ni pamoja na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

 
Vifaa mbalimbali vya Tehama zikiwemo Kompyuta, UPS na Projector kwa ajili ya kugawiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya umma 18.

“Nipende kuwasihi watumishi wote wa Wizara ya Elimu na hasa Idara ya manunuzi   kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni  wakati wa kutekeleza majukumu."

Vyuo vya Ualimu vya Umma ambavyo vimepata vifaa hivyo ni pamoja na Dawaka, Ilonga, Mandaka, Mhonda, Murutunguru, Mamire, Ndala, Singachini, Shinyanga na Vikindu.

Kaimu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe akizungumza na watumishi wa Wizara (hawapo) pichani wakati wa hafla ya kugawa vifaa vya Tehema mkoani Dodoma.


Vyuo vingine ni Patandi, Tarime, Mpuguso, Sumbawanga, Mpwapwa, Tukuyu , Morogoro na Korogwe.




Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ualimu nchini Augustino Sahili ameiomba serikali kuharakisha kukamilisha mpango wa kuunganisha vyuo vyote vya Ualimu vya umma na Mkongo wa Taifa.
Baadhi ya Wakuu wa Vyuo vya Ualimu wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu Profesa James Mdoe (hayupo pichani) wakati wa ugawaji wa vifaa vya Tehama kwa Vyuo vya Ualimu. Hafla hiyo imefanyikia mkoani Dodoma.

Alhamisi, 7 Machi 2019

WAZIRI NDALICHAKO ASEMA SAYANSI NA TEKNOLOJIA NI MUHIMU KATIKA UKUAJI WA UCHUMI


Serikali imewataka  wabunifu nchini kujikita katika  kuangalia shughuli za ambazo zinafanyika katika mazingira yao na wabuni jinsi ya kuzirahisisha kwa kutumia Sayansi na kiteknolojia ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi nchini.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Ilboru Maximillian Masesa akitoa maelezo kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako  juu ya kifaa cha kubaini wanafunzi ambao wanatumia simu shuleni alichobuni.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako katika kilele cha Mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu mjini Dodoma. Waziri Ndalichako  pia aliongeza kuwa eneo la Sayansi na Teknolojia ni muhimu kwa taifa na likitumika vyema litasaidia  kuongeza uzalishaji na Kurahisisha utekelezaji wa mambo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

“Kwa muda mrefu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuwa ikisimamia zaidi Elimu kuliko masuala ya Sayansi na ubunifu hivyo ni vyema wabunifu waendelee kujitokeza  zaidi na wajikitike katika  ikubuni mbinu za kurahisisha mifumo ya shughuli mbalimbali za kijamii  ikiwemo Kilimo, ufugaji na njia bora za upatikanaji wa maji”, alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiangalia ubunifu wa injini ya Ndege  uliofanywa na Emmanuel Chibula kutoka Musoma, Mkoani Mara wakati wa kilele cha mashindano ya kitaifa ya sayansi, teknolojia na Ubunifu yaliyofanyika Jijini Dodoma.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Profesa James Mdoe amesema  lengo  la Mashindano hayo yaliyohusisha wabunifu kutoka  ngazi mbali za Elimu ni kuibua ubunifu, umahiri, kuchochea ugunduzi kwa lengo la kukuza matumizi ya Sayansi na Teknolojia katika maendeleo.
Wanafunzi mbalimbali wa Shule za Msingi na baadhi ya Wananchi wakifuatilia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere.

Mashindano hayo  yalifunguliwa rasmi na Naibu Waziri Mhe. William Ole Nasha Machi 5, 2019 na leo yamefikia kilele ambapo washindi mbalimbali walipata zawadi za fedha na kutunukiwa vyeti.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na washiriki mbalimbali hawapo pichani wakati wa kufunga mashindano ya kitaifa ya kitaifa ya sayansi, teknolojia na Ubunifu yaliyofanyika Jijini Dodoma.

Kauli mbiu ya mashindano hayo kwa mwaka huu ni " kukuza ujuzi na ubunifu kwa uchumi wa viwanda".
Wanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji nchini NIT wabuni gari lisilotumia injini, na badala yake linatumia umeme kuendesha mifumo yake. Pichani Waziri akiwa kwenye gari hilo akipewa maelezo ya namna gari hilo linavyofanya kazi.