Ijumaa, 18 Oktoba 2019
Alhamisi, 17 Oktoba 2019
WAZIRI NDALICHAKO ATAKA MKUU WA SHULE KASANGEZI KUHAMISHWA
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako ametilia shaka matumizi ya fedha za serikali
zaidi ya shilingi milioni mia tano zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi na
ukarabati wa shule ya sekondari Kasangezi iliyopo wilayani Kasulu mkoani
Kigoma.
Akizungumza mara baada ya
kukagua utekelezaji wa mradi huo waziri Ndalichako amesema shule hiyo imepatiwa
zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 4,
mabweni 4 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 katika kila moja, matundu ya
vyoo 10, bwalo pamoja na ukarabati wa maabara.
Ndalichako amesema kazi iliyofanyika haiendani na fedha
iliyotolewa kutokana na miundombinu hiyo kujengwa chini ya Kiwango.
“Milango ya madarasa na hata
ya mabweni mmetengeneza kwa mbao laini tofauti na BOQ pamoja na kuwa laini ina
uwazi hii nataka itolewe, tazama sakafu imeshaharibika hapa hata mwaka
haujaisha mabweni mliambiwa ya watu themanini mmejenga ya watu sitini"
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiangalia mlango wa
darasa ambao umetengenezwa kwa mbao laini kinyume cha taratibu katika shule ya
sekondari Kasangezi
Kufuatia hali hiyo ndalichako
ameagiza kuwa ujenzi wa mabweni urudiwe kwa kuzingatia BoQ na ameaguza ujenzi
huo uwe umekamilika ifikapo desemba.
"Nitakuja mwenyewe
mwezi wa kwanza kukagua kama hayo yatakuwa hayajatekelezwa mengine yatafuata,”
amesema waziri Ndalichako.
Aidha waziri Ndalichako
amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya kumuondoa
mara moja shuleni hapo mkuu wa shule hiyo kwa kushindwa kusimamia vizuri kazi hiyo na hivyo kuisababishia
hasara serikali.
“Kwanza ujenzi wa mara ya
kwanza hata matofali hukununua ulichukua kwenye benki ya wananchi na tayari
nilikuwa nimeleta fedha sasa kwanini hukujiongeza hata ukarekebisha ofisi ya
Mkuu wa Shule ambayo iko katika hali isiyoridhisha vitu vingine ni kudhalilisha
Serikali, Mkurugenzi muahamishe huyu katika shule hii,” alisema waziri
Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akikagua maendeleo ya ujenzi wa moja ya bweni katika shule ya
sekondari Kasangezi iliyoko Halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Waziri Ndalichako pia
ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kasulu
kufuatilia muenendo wa upatikanaji wa madawati miamoja themanini
yaliyonunuliwa katika mradi huo kama yametimia na yamenunuliwa kwa kufuata
utaratibu.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Kasulu Kanali Saimon Anange amekiri kuwepo uzembe katika kusimamia
miradi hiyo na kumuhakikishia waziri Ndalichako kuwa ofisi yake itafanyia kazi
maelekezo yote aliyoyatoa katika ziara hiyo.
Waziri wa Elimu Sayansi na
Teknolijia Prof. Joyce Ndalichako yupo mkoani Kigoma Kwa ziara ya Kikazi
akikagua miradi ya elimu inatekelezwa kupitia fedha za Programu ya lipa kwa
matokeo EP4R.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua mlago wa darasa ambao umetumia mbao laini tofauti na maelekezo katika shule ya sekondari Kasangezi.
Jumatano, 16 Oktoba 2019
WAZIRI NDALICHAKO ATOA SIKU 15 KWA MSHAURI ELEKEZI BICO KUFANYA TATHMINI YA GHARAMA ZA UJENZI CHUO CHA UALIMU KABANGA
Wakati Mradi wa ujenzi wa
Chuo cha Ualimu Kabanga kilichopo Wilayani Kasulu mkoani Kigoma ukiendelea kwa kusuasua Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ametoa siku 15 kwa
Mshauri Elekezi BICO kupitia upya
gharama za ujenzi wa mradi huo ambazo ni
zaidi ya shilingi bilioni kumi
ili kujiridhisha kama fedha hiyo inaendana na ukubwa wa mradi.
Prof. Ndalichako ametoa
agizo hilo mara baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo ambapo pamoja na
kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi ametilia shaka gharama ya ujenzi ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni
kumi kutumika ndivyo sivyo kutokana na aina ya majengo yanayojengwa katika chuo
hicho kuwa ya thamani ndogo.
"Hivi ni vighorofa
mtoto na narudia ni vighorofa mtoto huwezi kuniambia kwamba majengo haya ambayo
kwanza ni machache, pili siyo ghorofa zile kubwa kama tulizojenga katika miradi
mingine tena kwa gharama ndogo ya shilingi bilioni sita zinazidiwa na vighorofa
hivi hapa kuna kitu hakipo sawa nataka ndani ya siku kumi na tano gharama za
mradi zipitiwe upya kwa kila jengo na nipewe taarifa vinginevyo mratibu wa
miradi hii utafute kazi nyingine," alisema Prof. Ndalichako.
Injinia wa mradi wa ujenzi
wa Chuo cha Ualimu Kabanga akimuonesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof Joyce Ndalichako namna chuo cha Ualimu Kabanga kitakavyoonekana baada ya
ujenzi kukamilika
Kuhusu kusuasua kwa Mradi
Waziri Ndalichako amemtaka Mkandarasi huyo ambaye ni Kampuni ya SUMA JKT
kuongeza kasi ya kufanya kazi akisisitiza ziletwe mashine za kisasa ambazo
zitarahisisha kazi pamoja na kuongeza vibarua kwenye eneo la kazi.
"Huwezi kutekeleza
mradi wa zaidi ya shilingi bilioni kumi kama nyumba yako unayojenga, yaani una
kamashine kamoja tena kakusukuma,vibarua wenyewe inaonekana umewaleta leo baada
ya kusikia nakuja kukagua, hii haikubaliki tunataka kazi ifanyike usiku na
mchana kwa sababu pesa zipo lazima mradi ukamilike haraka," alisema
Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu,
Kabanga unaojengwa na Wizara kupitia Mradi wa TESP wilayani Kasulu mkoani Kigoma
Mapema akitoa taarifa
ya mradi huo, Kaimu Mkuu wa Kanda ya Ujenzi SUMA JKT, Luteni Kanali
Onesmo Njau amesema mpaka sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia thelathini na
kudai kukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo
usumbufu wa kupata vifaa vya ujenzi kama saruji na mchanga.
"Mheshimiwa Waziri
tulikuwa tukitegemea kupata saruji kwa kampuni ya Dangote lakini kwa sasa
inabidi tufuate wenyewe Dodoma na hivyo kutumia muda mwingi kusubiri vifaa
vifike kwenye eneo la mradi," alisema Kanali Njau.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga
Kasulu Mkoani Kigoma
Naye mshauri elekezi wa
mradi huo kutoka BICO, Fred Munishi amekiri kuwa kazi inasuasua na kusema kuwa
tayari ametoa maelekezo kwa Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi taarifa ambayo
hata hivyo imeonekana kukinzana na taarifa ya Mkandarasi na hivyo kutakiwa
kufanya kazi kwa karibu na Mkandarasi.
"Inaonekana hapa hakuna
maelewano mazuri baina ya Mkandarasi na mshauri elekezi, sitaki mivutano kazini
kaeni pamoja fanyeni kazi ya serikali na mkiendelea hivi tutawaondoa,"
alisema Waziri Ndalichako.
Akiwa katika Halmashauri ya
wilaya ya Kasulu, Waziri Ndalichako pia amekagua miradi mingine minne ya elimu
katika shule za sekondari na msingi za Kigodya, Ruhita, Nyantare na Kasyenene na kueleza kuridhishwa na kazi
huku akisisitiza kuwa serikali inatoa fedha ili kuona matokeo.
Katika ziara hiyo Waziri
Ndalichako aliambatana pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Dkt. AveMaria
Semakafu pamoja na Mratibu wa Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo pamoja na ule
wa TESP.
Muonekano
wa sasa wa hatua ya ujenzi wa baadhi ya majengo katika eneo la mradi wa Chuo
cha Ualimu Kabanga wilani Kasulu Mkoani Kigoma
USIMAMIZI MBOVU WA MIRADI YA ELIMU BUHIGWE WAMKERA WAZIRI NDALICHAKO
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameonesha kukerwa na usimamizi mbovu wa
miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma na kumuagiza
Katibu Mkuu wa Wizara anayoisimamia, Dkt. Leonard Akwilapo kuleta wataalamu
watakaofanya ukaguzi maalum wa utekelezaji wa miradi ya elimu katika wilaya
hiyo.
Waziri Ndalichako ametoa
kauli hiyo Wilayani Buhigwe mkoani
Kigoma mara baada ya kukagua baadhi ya
miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara kupitia Mpango wa Lipa
Kulingana na Matokeo (EP4R)na kubaini uwepo wa kasoro kadhaa ikiwemo matumizi
ya vifaa vya ujenzi vilivyo chini ya Kiwango na
majengo ya shule ya Msingi ya mfano Bwega kutofautiana na ramani iliyopendekezwa na
wizara.
"Kwa ujumla usimamizi
wa Miradi katika wilaya ya Buhigwe siyo
mzuri, maafisa elimu hawawajibiki katika kuangalia kazi zao, unakuta kazi
zimefanyika hovyo, watu hawafuatilii," alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia akikagua moja ya nyumba za walimu katika Shule ya Msingi Kasumo
iliyoko wilayani Buhigwe mkoani Kigoma
Waziri Ndalichako amesema
Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe hatimizi wajibu wake ipasavyo kwa
kuwa ameshindwa kusimamia miradi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa na kuruhusu
matumizi ya vifaa vya ujenzi visivyo na ubora lakini pia ameshindwa kufuata
ramani katika ujenzi wa majengo ya shule
ya msingi ya mfano inayojengwa wilayani humo.
Kiongozi huyo amesema
tayari amewasiliana na Katibu Mkuu wa
Wizara, Dkt. Leonard Akwilapo ili ufanyike ukaguzi wa kina katika miradi ya
elimu Wilaya ya Buhigwe lengo likiwa ni kubaini
mapungufu na iwapo kuna mtu kafanya uzembe kwa manufaa yake awajibike.
"Inabidi kabla ya
kuleta fedha nyingine za miradi ya elimu wilayani Buhigwe ije timu ya watalaamu
mainjinia wachunguze walinganishe BoQ na kilichofanyika, haiwezekani turuhusu
uzembe kama huu kuendelea kwenye miradi inayotumia fedha ya wananchi wanyonge,"
aliongeza Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akionesha dosari kwenye jengo la maabara la
shule ya sekondari Janda wakati akikagua miradi ya elimu inayotekelezwa katika
shule hiyo na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R)
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayanalina amemshukuru Waziri Ndalichako kwa
ziara yake wilayani humo na kusema kuwa
mapungufu yote yaliyobainika tayari
Kamati yake imeyatolea maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na
kwamba zoezi linaloendelea ni kuwachukulia hatua wahusika.
"Kamati ya Usalama ya
wilaya ilibaini mapungufu katika miradi mbalimbali na tulitoa maelekezo kupitia
kwa Mkurugenzi na vyombo vyetu
vilishaagizwa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki," amesema Mkuu
wa Wilaya hiyo, Ngayalina.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa maabara unaoendelea katika
shule ya sekondari Janda iliyoko Buhigwe Mkoani Kigoma
Naye Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo, Anosta Nyamoga amesema ofisi yake tayari imemfukuza kazi
fundi aliyekuwa na mkataba wa kufanya ukarabati na ujenzi wa vyumba vya
madarasa katika Shule ya Sekondari Janda kutokana na kufanya kazi hiyo chini ya
viwango na kuahidi kuzifanyia kazi kasoro zote ambazo zimebainishwa na Waziri
Ndalichako.
Akiwa wilayani Buhigwe
Waziri Ndalichako amekagua miradi ya elimu katika shule ya msingi Bwega, shule
ya sekondari Janda, shule ya sekondari
Muyama na shule ya msingi Kasumo ambayo kwa pamoja inatarajia kugharimu zaidi
ya shilingi bilioni moja.
Waziri Ndalichako yuko
Mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya Elimu katika Halmashauri ya
Wilaya ya Buhigwe na Halmashauri ya Mji Kasulu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua moja ya dawati lililoko katika Shule
ya Sekondari Muyama mara baada ya kukagua ujenzi wa darasa hilo
Jumanne, 15 Oktoba 2019
Ijumaa, 4 Oktoba 2019
WAZIRI NDALICHAKO AWAASA WANAFUNZI WANAOMALIZA KIDATO CHA NNE KUWA NA MAADILI
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako
amesema elimu bila nidhamu na maadili haiwezi kusaidia kufanikiwa katika
maisha.
Waziri Ndalichako ameyasema
hayo wakati wa mahafali ya 32 ya shule ya sekondari Suji iliyoko wilayani Same mkoani Kilimanjaro.
Amesema katika maisha
ili mtu afanikiwe ni lazima awe na nidhamu ya kufanya kazi aliyonayo kwa wakati
ikiwa ni pamoja na kuheshimu mamlaka na hata watu walio chini yako na kuwataka
wanafunzi kuyaishi hayo mara baada ya
kumaliza elimu ya kidato cha nne
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akimtunuku cheti cha kuhitimu kidato cha Nne
Mwanafunzi Tajiel Omary wa Shule ya Sekondari Suji iliyoko wilayani Same Mkoani
Kilomanjaro
Kiongozi huyo
ameupongeza uongozi wa shule ya sekondari Suji kwa kuwalea wanafunzi katika
maadili mema ya kumjua Mungu na kuwapongeza kwa
kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya Kidato cha nne na
cha sita.
Ndalichako amewataka
wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo yao ili wengi zaidi waweze kufaulu kwa
kupata daraja la kwanza.
"Pamoja na
ufaulu wenu mzuri lakini nataka daraja
la kwanza ziongezeke, kwa sababu ukiangalia matokeo ya shule hii kwa miaka
mitatu mfululizo kuanzia 2016 hadi 2018
hata kama hakuna daraja la nne lakini wanaopata daraja la kwanza ni wachache
hivyo ongezeni juhudi ili ili huku kwenye daraja la kwanza muongezeke,"alisema
Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa mahafali ya 32 ya Shule
ya Sekondari Suji iliyoko Wilayani Same mkoani kilimanjaro
Amewataka wanafunzi
kuwa na uzalendo na nchi yao ikiwa ni pamoja na kuzilinda tunu Taifa
zilizoachwa na waasisi waxtaifa letu
ambazo ni pamoja na amani, umoja na
mshikamano.
"Mnaona kazi
kubwa ambayo Rais wetu wa Awamu ya Tano anaifanya anahakikisha rasilimali za nchi
haziibiwi zinawanufaisha watu wote hivyo mnapomaliza mkamuunge mkono kwa
kufanya kazi kwa bidii ili dhamira yake ni kuona nchi yetu inapata maendeleo
inafanikiwa ," alisema Waziri Ndalichako.
Waziri Ndalichako
ametumia fursa hiyo kuwatakia heri na mafanikio wanafunzi wote wa kidato cha
nne wanaotarajia kuanza mitihani yao Mwezi Novemba mwaka huu.
Baadhi ya wahitimu wa Kidato
cha Nne katika Shule ya Sekondari Suji ya Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro
wakiingia kwenye mahafali yaliyofanyika katika viawanja vya shule hiyo
Kwa upande wake Mkuu
wa Wilaya ya Same Rozimary Staki amesema Wilaya ya same ina shule za sekondari
53 ambapo 17 zinamilikiwa na watu binafsi pamoja na taasisi za dini.
Staki amesema kama
Wilaya wamekuwa wakishirikia na na Viongozi wa Dini katika kuelimisha mabinti
umuhimu wa kujitambua wanapokuwa shuleni.
Nae Mkuu wa Shule ya
Sekondari Suji Silnani Dismas amesema shule hiyo pamoja na kusisitiza masoma inawalea wanafunzi katika maadili na nidhamu ya hali
ya juu kwa kuwa ni ya kanisa.
Dismas amesema shule
hiyo ina wanafunzi takribani 568 na mafanikio wanayojivunia ni kuendelea
kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akisalimiana na Walimu wa shule ya Sekondari
Suji mara baada ya kuwasili katika shule hiyo kwa ajili ya mahahafali ya 32 ya
shule hiyo.
Mwanafunzi bora
katika masomo Tajiel Omary ambae anatarajia kuhitimu masomo ya kidato cha nne mwaka
huu amasema ufauli katika masomo unatokana na juhudi ambazo amekuwa akizifanya
katika masomo ikiwa ni pamoja na kumuomba Mungu ili malengo yake yatimie.
Waziri Ndalichako pia
alitembelea shule ya sekondari Makanya na kuongea na wanafunzi ambapo
amewatakia pia heri katika mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne Mwezi Novemba
mwaka huu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akifurahi pamoja na Wanafunzi wa Shule ya
Sekondari Makanya iliyopo Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)