Serikali imesema inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na vyuo binafsi katika kuleta maendeleo ya elimu ya juu kikiwemo Chuo Kikuu cha St. John’s cha hapa nchini.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako wakati wa mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu cha St. John’s ambapo amesema kuwepo kwa vyuo binafsi hapa nchini kunasaidia na kuwezesha nchi yetu kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaopata mafunzo ya elimu ya juu.
Waziri Ndalichako amesema Chuo hicho kimekuwa kikitoa mchango mkubwa katika utayarishaji wa wataalamu katika fani mbalimbali ikiwemo fani ya ufamasia, uuguzi, ualimu wa Sayansi na Sanaa, kilimo, usimamizi wa fedha, uendeshaji katika utawala, masoko, uhasibu na wataalamu wa maabara.
“Nimeelezwa kuwa tangu chuo hichi kuanza mwaka 2007 hadi hivi sasa kimeweza kutoa wahitimu wasiopuungua elfu kumi na mbili, huu ni mchango mkubwa kwa Taifa letu, hongereni sana,” alisema Prof Ndalichako.
Amewapongeza wahadhiri wa Chuo hicho kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ya kuwafundisha vijana ambapo amewataka kuendelea kuwaandaa vema wahitimu ili wakawe chachu na mfano wa kuigwa katika jamii wanazokwenda kuishi baada ya kuhitimu masomo yao.
“Nimefurahi kusikia kuwa Chuo hiki pamoja na masuala ya kitaaluma kinatilia mkazo suala la maadili, kinasisitiza umuhimu wa wanachuo kumuheshimu Mungu, kuwa waadilifu, kufanya kazi kwa bidii na kuwa tayari kuhudumia wengine,” aliongeza Prof. Ndalichako.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amesema suala la utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya juu ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaostahili kupata mikopo wanapata na kuwawezesha kusoma bila changamoto yoyote.
“Nimefarijika kusikia kwamba idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo katika chuo cha St. John’s imeongezeka na kwamba mikopo hiyo inatoka kwa wakati, na hii niwaambie ukweli ni mpango wa Mhe. Rais. Mtakumbuka wakati akifanya kampeni aliahidi na kueleza namna alivyokuwa akisononeka kuona watoto wa kitanzania, wanafunzi wa elimu ya Juu walivyokuwa wakihangaika kupata fedha za mikopo, hivyo jambo la kwanza aliliolifanya alipoingia madarakani ni kuongeza kiasi cha fedha kinachotolewa kwa ajili ya mikopo kutoka bilioni 341 mwaka 2014/15 na sasa fedha zilizotengwa kwa mwaka 2019/20 ni sh bilioni 450,” alisema Waziri Ndalichako.
Waziri Ndalichako aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatoa fedha za mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa wakati akitolea mfano wanafunzi ambao wameanza masomo mwanzoni mwa mwezi Novemba 2019 Serikali imetoa fedha zao tangu mwezi Septemba.
“Hadi kufikia Oktoba 15, 2019 Serikali ilikuwa imekwishatoa jumla ya sh bilioni 185 sawa na asilimia 41 ya fedha ambazo zimepangwa kwa ajili ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka 2019/20,” alisema Waziri Ndalichako.
Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuviagiza vyuo vyote nchini ambavyo kwa namna moja au nyingine bado havijatoa fedha kwa wanafunzi kutoa fedha hizo kwani Serikali inatoa fedha kwa ajili ya wanafunzi na sio kwa ajili ya vyuo.
Aidha Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi wanaohitimu masomo ya elimu ya juu kuwa mabalozi wazuri wa vyuo walivyosoma na Taifa kwa ujumla huku akiwataka kuwa wazalendo na watu ambao wanaweka maslahi ya taifa mbele na kupinga vitendo vya aina yoyote vyenye lengo la kuvuruga amani na mshikamano wa Taifa letu.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St.John’s, Prof. Yohana Msanjila amesema wanafunzi wanaohitimu katika Chuo hicho kwa mwaka 2019 wako 1,730 huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza idadi ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wanaopata mikopo ikiwa ni pamoja na kuwa na usimamizi mzuri wa utoaji mikopo ya elimu ya juu.
“Fedha za wanafunzi na ada zao zinatolewa mapema tofauti na miaka ya nyuma. Nakuomba mgeni rasmi Mhe. Prof. Joyce Ndalichako utufikishie pongezi zetu kwa Mhe. Rais kwamba siku hizi fedha za mikopo na ada za wanafunzi zinafika kwa wakati na hii imesaidia kudumisha utulivu chuoni. Hongera kwa Serikali yetu, hongera Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu,” alisema Prof Msanjila.
Mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu cha St. John’s kwa mwaka 2019 yalikuwa na Kauli mbiu isemayo “Udijitalishaji wa Elimu ya Juu kwa Vyuo binafsi: Kiungo Bora kwa Uchumi wa Viwanda.”