Jumatatu, 17 Juni 2019

NAIBU KATIBU MKUU MDOE ASEMA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA NI MSINGI WA UFANISI KATIKA UTENDAJI KAZI

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amesema maadili ya utumishi wa umma ni msingi na nguzo ya utendaji wa ufanisi katika utumishi wa umma.

Profesa Mdoe ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maadili kwa watumishi wa kada saidizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo amesema lengo la kufanya mafunzo hayo ni kukumbushana kuhusu maadili katika utumishi wa umma, utoaji wa huduma bora kwa mteja na utunzaji wa siri na nyaraka za serikali.
Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maadili kwa watumishi wa kada saidizi yaliyofanyika jijini Dodoma Juni 17, 2019. Amesisitiza kuwa na
maadili mahali pa kazi ili kuleta ufanisi wa kazi.
"Suala la maadili katika utumishi wa umma si suala la hiari kwa yeyote aliyeajiriwa na kwamba inapotokea mtumishi akatenda kinyume atachukuliwa hatua kulingana na sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi zilizopo," alisisitiza Profesa Mdoe.

Naibu Katibu Mkuu Mdoe amesema utumishi unaozingatia maadili hujidhihirisha pale mtumishi anapotoa huduma kwa wananchi bila upendeleo, rushwa, ubaguzi, staha, uadilifu, uwazi na kufanya kazi kwa bidii.

Aliongeza kuwa suala la uadilifu linakwenda sambamba na utunzaji wa siri na nyaraka za serikali na zile za wateja wanaotumia huduma za wizara na linapaswa kuzingatiwa na kila mtumishi wa umma katika nafasi yake huku akisisitiza matumizi sahihi ya teknolojia katika utendaji.
Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wanaoshiriki mafunzo ya maadili wakifuatilia Hotuba ya ufunguzi ya Naibu Katibu Mkuu, Prof. James Mdoe.
"Watumishi tujihadhari na matumizi mabaya ya teknolojia sio kila kitu unachokiona ofisini unakipiga picha na kukisambaza, teknolojia itumike na maadili ikunufaishe na sio ikuangamize,"aliongeza Profesa Mdoe.

Prof. Mdoe amemtaka kila mtumishi kuona fahari ya kuhudumu katika utumishi wa umma na lengo kubwa katika utendaji liwe kutoa huduma inayokidhi mahitaji ya watumiaji wa huduma inayotolewa.

Awali akizungumza katika mafunzo hayo Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Sebastian Inoshi alimweleza Naibu Katibu Mkuu kuwa utoaji wa mafunzo hayo ni muendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa wizara kwa mwaka 2018/19 wa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi kwa ajili ya kuwajengea uwezo ili kuwasaidia kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kiofisi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi walioshiriki mafunzo ya maadili yaliyofanyika jijini Dodoma Juni 17, 2019.

Ijumaa, 14 Juni 2019

WAZIRI NDALICHAKO ATAKA VIONGOZI WA ELIMU KUTAMBUA JUHUDI ZINAZOFANYWA NA WALIMU NA WANAFUNZI KATIKA MASOMO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezitaka shule na wanafunzi kuendeleza juhudi katika masoma ili kujenga Taifa la watu waliosheheni ujuzi na maarifa ambao unahitajika kwa ajili ya maendeleo endelevu nchini.

Waziri Ndalichako ametoa wito huo jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya siku ya elimu ambayo yamekwenda sambamba na hafla ya utoaji tuzo kwa shule na wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha nne na cha sita waliofanya vizuri zaidi katika mitihani ya kitaifa ya mwaka 2018.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisisitiza jambo wakati wa maadhimisho ya siku ya elimu yaliyofanyika Jijini Dodoma. Maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na hafla ya utoaji tuzo kwa Shule na wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari waliofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwa mwaka 2018. 
Kiongozi huyo amewataka wanafunzi waliopata tuzo hizo kuendeleza juhudi katika masomo yao wanayoendelea nayo huku akiwataka viongozi wa elimu katika ngazi zote kujenga utamaduni wa kuwapongeza walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo kwani inatoa chachu ya kuendele kufanya vizuri zaidi.

“Haya matokeo ya wanafunzi sio matokeo ya kupika yanatokana na juhudi zao wenyewe, walimu na wazazi wao katika kusimamia ikiwa ni pamoja na juhudi za Serikali katika kuhakikisha wanakuwa na mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia,” alisema Waziri Ndalichako

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akitoa zawadi kwa baadhi ya shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwa mwaka 2018.
Aidha Waziri Ndalichako amesema Wizara yake inatambua umuhimu wa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili kupata matokeo mazuri ambapo katika mwaka wa fedha 2018/19 Serikali imejenga madarasa 1208, mabweni 222 matundu ya vyoo 2,141 na nyumba za walimu takribani 198, huku ikiimarisha huduma za maji kwenye shule ambazo zilikuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji na kupelekea wanafunzi kulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Pia Waziri Ndalichako amesema Wizara inatambua umuhimu wa kuwaandaa walimu katika mazingira yaliyo mazuri hivyo imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika vyuo hivyo.

“Kama ambavyo mmeshuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa katika ziara yake ya mikoa ya kusini mwa nchi yetu aliweza kufika katika vyuo vya ualimu Kitangali, Mpuguso ambapo hii ni sehemu ya miradi mikubwa ambyo inafanywa na Wizara na miradi aliyoizindua ni sehemu ya miradi mikubwa minne inayotekelezwa katika vyuo vya ualimu Shinyanga, Mpuguso, Kitangali pamoja na Ndala, tunafanya kweli hatubeep,” alisisitiza Waziri Ndalichako.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akitoa zawadi ya cheti na fedha kwa mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya Kitaifa kwa mwaka 2018. 
Awali akizungumza katika hafla hiyo Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa alisema utoaji wa tuzo kwa shule na Wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya Taifa ni miongoni mwa shughuli zinazotekelezwa na Mradi wa Lipa Kulinga na Matokeo katika Elimu (EP4R) ambapo kwa mwaka 2019 zawadi zimetolewa kwa jumla ya shule 3,916 (Msingi 3,135 na Sekondari 781) zilizofanya vizuri na zilizoongeza ufaulu kwa asilimia 10 pamoja na wanafunzi 29 wa shule za Sekondari kidato cha nne na cha sita.

1.      KAMISHNA WA ELIMU LYABWENE MTAHABWA AKIZUNGUMZA WAKATI WA HAFLA YA UTOAJI TUZO KWA SHULE NA WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI KATIKA MITIHANI YA KITAIFA YA MWAKA 2018.

Jumapili, 2 Juni 2019

NDALICHAKO ATAKA MFUMO WA ELIMU KATIKA VYUO VIKUU KUANDAA VIJANA WENYE MAWAZO NA MTAZAMO CHANYA NA WA KIMAENDELEO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewaasa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Iringa kutumia mfumo wa elimu kuandaa vijana ambao watakuwa na mtazamo chanya  na mawazo ya kimaendeleo  yanayolenga kuja na majawabu ya changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika jamii, ametaka vijana wajengwe katika kuona fursa zaidi.

Amesema hayo katika siku ya maadhimisho ya Kitivo cha Sayansi na Elimu katika Chuo Kikuu cha Iringa ambapo alikuwa Mgeni Rasmi katika siku hiyo ambayo huadhimishwa kila mwaka mkoani Iringa. Ndalichako amewataka vijana wanaosoma katika Chuo hicho kusoma kwa bidii ili  elimu wanayoipata iweze kuwasaidia wao binafsi na jamii zinazowazunguka.

“Serikali yenu sikivu inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati na kuboresha elimu nchini, kwa hili tumpongeze Rais wetu, na kama kauli mbiu ya hapa kazi inavyosema, Rais na sisi  tunachapa kazi  ninyi kazi yenu ni kusoma kwa bidii ili mkimaliza muweze kushiriki moja kwa moja katika kujenga uchumi katika taifa letu.”
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wanajumuiya wa Chuo Kikuu Iringa  wakati wa maadhimisho ya  siku ya Kitivo cha Sayansi na Elimu katika Chuo Kikuu cha hicho.

Ndalichako amesema Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya usimamizi wa elimu ya juu kupitia Tume ya Vyuo Vikuu kwa lengo la kuhakikisha Vyuo vinatoa wahitimu bora na wenye sifa na ujuzi kwa ajili ya kuajiriwa na vile vile wenye ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na amewataka Uongozi wa chuo hicho kuhakikisha kasoro zilizotolewa na TCU katika baadhi ya programu zao ambazo zimesitishwa zinarekebishwa kwa haraka ili zipate ithibati.  Ametumia nafasi hiyo pia kuwataka Vyuo Vikuu nchini kufuata Kanuni, Sheria na taratibu za uendeshajI Vyuo wakati wote.

 Akiwa chuoni hapo ameongezea kuwa Serikali inathamini mchango wa sekta binafsi katika kutoa elimu huku akitolea mfano uwekezaji uliofanywa katika Chuo hicho na Serikali kwa  kutoa mitambo na vifaa mbalimbali vya Tehama vinavyowezesha utumiaji wa mkongo wa Taifa.

Awali akitembelea kituo atamizi cha chuo hicho, amepongeza juhudi mbalimbali zilizofanyika katika kituo hicho kwa kulea mawazo ya kibunifu hadi kufikia kutayarisha bidhaa, kuanzishwa biashara na kutoa mafunzo ya ujasiriamali na masoko kwa wanachuo na jamii inayowazunguka. Aidha amewataka vijana waliobuni bidhaa kuhakikisha  wanafuata taratibu za kurasimisha bidhaa zao.

Waziri Ndalichako amefurahishwa na uwezo mkubwa waliyouonesha wanafunzi wabunifu walio katika kituo hicho na kuwataka kuendelea na mawazo na mtazamo wa kijasiriamali ambapo amesema hayo ni matokeo halisi ya mafunzo yanayotolewa na chuo hicho katika Shahada ya Ujasiriamali na Masoko kwa vitendo yaani “Bachelor of Applied Marketing and Entrepreneurship.”
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiangalia bidhaa zilizotengenezwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa wakati wa Chuo Kikuu Iringa  wakati wa maadhimisho ya  siku ya Kitivo cha Sayansi na Elimu katika Chuo Kikuu cha hicho.
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Prof.  Ndelerio Urio, amesema mwaka huu chuo kina wanafunzi zaidi ya 3,215. Amemshukuru Waziri kwa kutembelea Chuo hicho na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kusaidia vyuo binafsi. Prof Urio  ameahidi kuendelea kusimamia ubora katika utoaji elimu ili kuendelea kutoa wahitimu bora akisistiza kuwa wataendelea kujitathmini kila wakati ili kuhakikisha wanakuwa na programu bunifu zinazokidhi mahitaji ya soko.

SERIKALI KUSAIDIA UANZISHWAJI WA KITUO CHA KUATAMIA UBUNIFU NA BIASHARA CHA CHUO KIKUU MZUMBE


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Prof. Joyce Ndalichako amesema Wizara yake iko tayari kusaidia kutafuta  rasilimali kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kuatamia Ubunifu na Biashara “Innovation and Business Incubation Centre “ cha Chuo Kikuu Mzumbe, ambacho kitatoa fursa kwa wanafunzi wanaosoma katika Chuo hicho na Vyuo vingine na vijana wengine wenye mawazo ya kiubunifu, ujasiriamali na biashara, kuyaboresha mawazo na shughuli zao za kiubunifu ili ziweze kuwa biashara kamili.

Waziri Ndalichako amesema hayo katika kilele cha kambi ya ujasiriamali ya Chuo Kikuu Mzumbe iliyofanyika katika Kampasi yake Kuu Morogoro ambapo amepongeza hatua hiyo ya kuanzishwa kwa kambi hiyo ambayo ni mara ya tatu inafanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017, huku akisema utaratibu huo ni tafsiri sahihi na kwa vitendo ya agenda ya Kitaifa ya kujenga Uchumi wa Viwanda.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiangalia bidhaa zilizotengenezwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakati wa  kilele cha kambi ya ujasiriamali ya Chuo hicho iliyofanyika katika Kampasi yake Kuu Morogoro
 “Nimefurahi sana leo kuona bidhaa na ubunifu wa hali ya juu hapa na kusikia kuwa Kambi hii imeendelea kuvutia watu wengi, wakiwemo wanafunzi, baadhi ya wafanyakazi na watu wengine kutoka jamii zinazotuzunguka, utaratibu huu utakuwa na faida ya muda mrefu kwa Chuo kwani wahitimu wenu watakuwa wameiva kinadharia na kivitendo, na wenye uwezo wa kujiajiri na kutengeneza ajira”.

Ndalichako amevitaka vyuo vingine kuiga mfano huu ambao unatoa fursa ya kukitangaza Chuo ambapo watanzania wataweza kujionea namna ambavyo fani mnazofundisha kama Uongozi wa Biashara, Ujasirimali, Uchumi na Mipango, TEHAMA, na zingine zinavyotayarisha wahitimu ambao wana mawazo ya kibunifu na ujasiriamali na mtazamo wa kibiashara.

Ndalichako amewataka Chuo Kikuu Mzumbe kuhahakisha kupitia kituo hicho atamizi kinawezesha wabunifu wao kushiriki katika mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU), kwa lengo la kuhamasisha ubunifu nchini yanayoratibiwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akionyesha kitabu kilichoandikwa na Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe mara baada ya kkizindua wakati wa  kilele cha kambi ya ujasiriamali ya Chuo hicho iliyofanyika katika Kampasi yake Kuu Morogoro
Akizungumza katika kilele hicho Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka amesema kambi hiyo inashirikisha wanafunzi wa Mzumbe na wengine, wahitimu wa Mzumbe ambao ni wajasiriamali. Ameongezea pia kuwa kupitia kambi hiyo wanafunzi wenye mawazo ya kibiashara pia hukutanishwa na wafanyabiashara walibobea na ili kupata uzoefu.  Kusiluka ameahidi kusimamia uanzishwaji wa haraka wa kituo atamizi kwani kitasaidia kukuza mawazo ya kibunifu kuwa biashara kubwa nchini zitakazo changia pato la Taifa.

Nae mzungumzaji Mkuu wa kambi ya Mwaka 2019. Ndugu Ahmed Lussasi ambae ni mhitimu wa Chuo kikuu Mzumbe  na Mwazilishi mwenza wa kampuni ya MAXOM AFRICA, kampuni inayofanya vizuri katika biashara, amesema anapongeza wazo la kituo atamizi na ameiomba Serikali kulipa kipaumbele , kwani biashara yao ilianza kwa kulelewa katika kituo atamizi na hatimae kukua.  Lusassi kama mmoja wa wahitimu amekitaka Chuo kuwa na mfumo mzuri wa kushirikisha wahitimu wake katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya Chuo hicho.

Katika kambi hiyo Ndalichako amezindua bidhaa mbalimbali zilizobuniwa na wanafunzi wabunifu na wajasiriamli katika chuo hicho, ikiwa ni pamoja na kitabu kilichoandikwa na mwanafunzi wa Chuo hicho. Kwa mwaka 2019 wanafunzi 48 wameandikisha mawazo yao ya kibunifu ili yaweze kuboreshwa.


CHUO KIKUU MZUMBE CHATIKIWA KUWEKA UTARATIBU MZURI ILI KUWEZESHA WANAFUNZI KUPATA MIKOPO KWA WAKATI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameanza ziara za kukutana na wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kupokea na kusikiliza maoni, mapendekezo na changamoto za wanafunzi hao kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi.
Waziri Ndalichako ameanza ziara hiyo katika Chuo Kikuu Mzumbe akiwa ameambatana na viongozi kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo ameuagiza uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kuandaa utaratibu utakaohakikisha wanafunzi wanaojitokeza kusaini nyaraka za mikopo mapema kuwezeshwa kupata fedha zao kwa wakati.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungmza na Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakati wa ziara yake ya kutembelea vyuo Vikuu na kuzungumza na wanafunzi
“Hili jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanasaini kwa wakati nakupa Rais wa wanafunzi, uwahamasishe wenzako kusaini mapema ili wapatiwe fedha kwa kuwa serikali haina tatizo la fedha na ndio sababu zinapelekwa kwa wakati katika Vyuo,” alisisitiza Waziri Prof. Ndalichako.
Awali, baadhi ya wanafunzi walimweleza Waziri kuwa wanachelewa kupokea fedha za mikopo zinazopelekwa chuoni hapo na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutokana na kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa kupata taarifa.
Ili kutatua changamoto zilizopo katika kupatikana kwa mikopo kwa wakati wanafunzi hao walipendekeza kuwepo kwa mikutano ya mara kwa mara kati ya Serikali ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili kujadili kwa pamoja changamoto zilizopo na kuzitafutia uvumbuzi kwa pamoja.
Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Hayupo Pichani) wakati wa ziara yake ya kutembelea vyuo Vikuu na kuzungumza na wanafunzi
Akitoa ufafanuzi, Makamu Mkuu wa chuo Prof. Lugano Kusiluka amesema Menejimenti ya chuo hicho imekua ikikutana na changamoto ya baadhi ya wanafunzi kutojitokeza kusaini nyaraka zinazohitajika kuthibitisha uwepo wao chuoni licha ya kukumbushwa mara kwa mara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) Prof. Charles Kihampa wameahidi kutoa ushirikiano kwa menejimenti za vyuo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mikopo kwa wakati.

Ijumaa, 31 Mei 2019

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KATIKA KUENDELEZA UJUZI


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Tate-Ole Nasha amefunga rasmi maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ambapo ameilielekeza baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi kuhakikisha maonesho hayo yanafanyika angalau kwa mwaka mara moja.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema kuwa Elimu ya Ufundi ni nyenzo inayomsaidia mtu kupambana na changamoto ikiwemo kujiajiri na siyo kusubiria kuajiriwa, hivyo kupitia mafunzo ya ufundi yanawaandaa wahitimu kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maisha.

Mhe. Ole Nasha amesema Serikali ya awamu ya Tano inapozungumzia Tanzania ya viwanda ni pamoja na kujiandaa kuhakikisha inakuwa na wataalamu wenye stadi na ujuzi.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungmza na wananchi (Hawapo Pichani)  wa Dodoma wakati wa kufunga maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo yaliyofanyika Jijini Dodoma
“Katika kufikia uchumi wa viwanda Serikali itaendelea kushirikiana na wadau na sekta mbalimbali katika kujiletea Maendeleo, na ili kufikia lengo hilo ni lazima tuwe na wataalamu wa kutosha ambao watasaidia kutatua changamoto mbalimbali,”alisistiza Mhe. Ole Nasha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Prof. John Kondoro amesema madhumuni ya maonesho hayo ni kutangaza Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu miongoni mwa washiriki.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha na Naibu Katibu Mkuu AveMaria Semakafu wakisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Skauti anayeshiriki katika Maonesho ya Kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo yaliyoratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo.
Prof. Kondoro amesema miongoni mwa changamoto ni pamoja na muda wa maandalizi kuwa mfupi na hivyo washiriki wengi kushindwa kujipanga na kuja kushiriki ameahidi kuwa baraza litajipanga ili kutoa fursa kwa washiriki wengi zaidi kushiriki katika maonyesho yajayo.

Kauli mbiu ni “Elimu ya Ufundi na Mafunzo kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda Tanzania”

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungumza na mmoja wa washiriki wa maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo wakati alipotembelea maonesho hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma