Jumatatu, 17 Juni 2019

NAIBU KATIBU MKUU MDOE ASEMA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA NI MSINGI WA UFANISI KATIKA UTENDAJI KAZI

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amesema maadili ya utumishi wa umma ni msingi na nguzo ya utendaji wa ufanisi katika utumishi wa umma.

Profesa Mdoe ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maadili kwa watumishi wa kada saidizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo amesema lengo la kufanya mafunzo hayo ni kukumbushana kuhusu maadili katika utumishi wa umma, utoaji wa huduma bora kwa mteja na utunzaji wa siri na nyaraka za serikali.
Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maadili kwa watumishi wa kada saidizi yaliyofanyika jijini Dodoma Juni 17, 2019. Amesisitiza kuwa na
maadili mahali pa kazi ili kuleta ufanisi wa kazi.
"Suala la maadili katika utumishi wa umma si suala la hiari kwa yeyote aliyeajiriwa na kwamba inapotokea mtumishi akatenda kinyume atachukuliwa hatua kulingana na sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi zilizopo," alisisitiza Profesa Mdoe.

Naibu Katibu Mkuu Mdoe amesema utumishi unaozingatia maadili hujidhihirisha pale mtumishi anapotoa huduma kwa wananchi bila upendeleo, rushwa, ubaguzi, staha, uadilifu, uwazi na kufanya kazi kwa bidii.

Aliongeza kuwa suala la uadilifu linakwenda sambamba na utunzaji wa siri na nyaraka za serikali na zile za wateja wanaotumia huduma za wizara na linapaswa kuzingatiwa na kila mtumishi wa umma katika nafasi yake huku akisisitiza matumizi sahihi ya teknolojia katika utendaji.
Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wanaoshiriki mafunzo ya maadili wakifuatilia Hotuba ya ufunguzi ya Naibu Katibu Mkuu, Prof. James Mdoe.
"Watumishi tujihadhari na matumizi mabaya ya teknolojia sio kila kitu unachokiona ofisini unakipiga picha na kukisambaza, teknolojia itumike na maadili ikunufaishe na sio ikuangamize,"aliongeza Profesa Mdoe.

Prof. Mdoe amemtaka kila mtumishi kuona fahari ya kuhudumu katika utumishi wa umma na lengo kubwa katika utendaji liwe kutoa huduma inayokidhi mahitaji ya watumiaji wa huduma inayotolewa.

Awali akizungumza katika mafunzo hayo Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Sebastian Inoshi alimweleza Naibu Katibu Mkuu kuwa utoaji wa mafunzo hayo ni muendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa wizara kwa mwaka 2018/19 wa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi kwa ajili ya kuwajengea uwezo ili kuwasaidia kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kiofisi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi walioshiriki mafunzo ya maadili yaliyofanyika jijini Dodoma Juni 17, 2019.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni