Ijumaa, 31 Mei 2019

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KATIKA KUENDELEZA UJUZI


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Tate-Ole Nasha amefunga rasmi maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ambapo ameilielekeza baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi kuhakikisha maonesho hayo yanafanyika angalau kwa mwaka mara moja.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema kuwa Elimu ya Ufundi ni nyenzo inayomsaidia mtu kupambana na changamoto ikiwemo kujiajiri na siyo kusubiria kuajiriwa, hivyo kupitia mafunzo ya ufundi yanawaandaa wahitimu kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maisha.

Mhe. Ole Nasha amesema Serikali ya awamu ya Tano inapozungumzia Tanzania ya viwanda ni pamoja na kujiandaa kuhakikisha inakuwa na wataalamu wenye stadi na ujuzi.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungmza na wananchi (Hawapo Pichani)  wa Dodoma wakati wa kufunga maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo yaliyofanyika Jijini Dodoma
“Katika kufikia uchumi wa viwanda Serikali itaendelea kushirikiana na wadau na sekta mbalimbali katika kujiletea Maendeleo, na ili kufikia lengo hilo ni lazima tuwe na wataalamu wa kutosha ambao watasaidia kutatua changamoto mbalimbali,”alisistiza Mhe. Ole Nasha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Prof. John Kondoro amesema madhumuni ya maonesho hayo ni kutangaza Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu miongoni mwa washiriki.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha na Naibu Katibu Mkuu AveMaria Semakafu wakisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Skauti anayeshiriki katika Maonesho ya Kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo yaliyoratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo.
Prof. Kondoro amesema miongoni mwa changamoto ni pamoja na muda wa maandalizi kuwa mfupi na hivyo washiriki wengi kushindwa kujipanga na kuja kushiriki ameahidi kuwa baraza litajipanga ili kutoa fursa kwa washiriki wengi zaidi kushiriki katika maonyesho yajayo.

Kauli mbiu ni “Elimu ya Ufundi na Mafunzo kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda Tanzania”

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungumza na mmoja wa washiriki wa maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo wakati alipotembelea maonesho hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni