Ijumaa, 14 Juni 2019

WAZIRI NDALICHAKO ATAKA VIONGOZI WA ELIMU KUTAMBUA JUHUDI ZINAZOFANYWA NA WALIMU NA WANAFUNZI KATIKA MASOMO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezitaka shule na wanafunzi kuendeleza juhudi katika masoma ili kujenga Taifa la watu waliosheheni ujuzi na maarifa ambao unahitajika kwa ajili ya maendeleo endelevu nchini.

Waziri Ndalichako ametoa wito huo jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya siku ya elimu ambayo yamekwenda sambamba na hafla ya utoaji tuzo kwa shule na wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha nne na cha sita waliofanya vizuri zaidi katika mitihani ya kitaifa ya mwaka 2018.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisisitiza jambo wakati wa maadhimisho ya siku ya elimu yaliyofanyika Jijini Dodoma. Maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na hafla ya utoaji tuzo kwa Shule na wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari waliofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwa mwaka 2018. 
Kiongozi huyo amewataka wanafunzi waliopata tuzo hizo kuendeleza juhudi katika masomo yao wanayoendelea nayo huku akiwataka viongozi wa elimu katika ngazi zote kujenga utamaduni wa kuwapongeza walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo kwani inatoa chachu ya kuendele kufanya vizuri zaidi.

“Haya matokeo ya wanafunzi sio matokeo ya kupika yanatokana na juhudi zao wenyewe, walimu na wazazi wao katika kusimamia ikiwa ni pamoja na juhudi za Serikali katika kuhakikisha wanakuwa na mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia,” alisema Waziri Ndalichako

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akitoa zawadi kwa baadhi ya shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwa mwaka 2018.
Aidha Waziri Ndalichako amesema Wizara yake inatambua umuhimu wa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili kupata matokeo mazuri ambapo katika mwaka wa fedha 2018/19 Serikali imejenga madarasa 1208, mabweni 222 matundu ya vyoo 2,141 na nyumba za walimu takribani 198, huku ikiimarisha huduma za maji kwenye shule ambazo zilikuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji na kupelekea wanafunzi kulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Pia Waziri Ndalichako amesema Wizara inatambua umuhimu wa kuwaandaa walimu katika mazingira yaliyo mazuri hivyo imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika vyuo hivyo.

“Kama ambavyo mmeshuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa katika ziara yake ya mikoa ya kusini mwa nchi yetu aliweza kufika katika vyuo vya ualimu Kitangali, Mpuguso ambapo hii ni sehemu ya miradi mikubwa ambyo inafanywa na Wizara na miradi aliyoizindua ni sehemu ya miradi mikubwa minne inayotekelezwa katika vyuo vya ualimu Shinyanga, Mpuguso, Kitangali pamoja na Ndala, tunafanya kweli hatubeep,” alisisitiza Waziri Ndalichako.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akitoa zawadi ya cheti na fedha kwa mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya Kitaifa kwa mwaka 2018. 
Awali akizungumza katika hafla hiyo Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa alisema utoaji wa tuzo kwa shule na Wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya Taifa ni miongoni mwa shughuli zinazotekelezwa na Mradi wa Lipa Kulinga na Matokeo katika Elimu (EP4R) ambapo kwa mwaka 2019 zawadi zimetolewa kwa jumla ya shule 3,916 (Msingi 3,135 na Sekondari 781) zilizofanya vizuri na zilizoongeza ufaulu kwa asilimia 10 pamoja na wanafunzi 29 wa shule za Sekondari kidato cha nne na cha sita.

1.      KAMISHNA WA ELIMU LYABWENE MTAHABWA AKIZUNGUMZA WAKATI WA HAFLA YA UTOAJI TUZO KWA SHULE NA WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI KATIKA MITIHANI YA KITAIFA YA MWAKA 2018.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.