Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameanza ziara za kukutana na wanafunzi wa
Elimu ya Juu ili kupokea na kusikiliza maoni, mapendekezo na changamoto za
wanafunzi hao kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi.
Waziri Ndalichako ameanza
ziara hiyo katika Chuo Kikuu Mzumbe akiwa ameambatana na viongozi kutoka Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo ameuagiza uongozi wa Chuo Kikuu
Mzumbe kuandaa utaratibu utakaohakikisha wanafunzi wanaojitokeza kusaini
nyaraka za mikopo mapema kuwezeshwa kupata fedha zao kwa wakati.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungmza na Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakati wa ziara yake ya kutembelea vyuo Vikuu na kuzungumza na wanafunzi
“Hili jukumu la kuhakikisha
wanafunzi wanasaini kwa wakati nakupa Rais wa wanafunzi, uwahamasishe wenzako
kusaini mapema ili wapatiwe fedha kwa kuwa serikali haina tatizo la fedha na
ndio sababu zinapelekwa kwa wakati katika Vyuo,” alisisitiza Waziri Prof.
Ndalichako.
Awali, baadhi ya wanafunzi
walimweleza Waziri kuwa wanachelewa kupokea fedha za mikopo zinazopelekwa chuoni
hapo na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
kutokana na kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa kupata taarifa.
Ili
kutatua changamoto zilizopo katika kupatikana kwa mikopo kwa wakati wanafunzi
hao walipendekeza kuwepo kwa mikutano ya mara kwa mara kati ya Serikali ya
Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili kujadili kwa pamoja
changamoto zilizopo na kuzitafutia uvumbuzi kwa pamoja.
Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Hayupo Pichani) wakati wa ziara yake ya kutembelea vyuo Vikuu na kuzungumza na wanafunzi
Akitoa ufafanuzi, Makamu
Mkuu wa chuo Prof. Lugano Kusiluka amesema Menejimenti ya chuo hicho imekua
ikikutana na changamoto ya baadhi ya wanafunzi kutojitokeza kusaini nyaraka zinazohitajika
kuthibitisha uwepo wao chuoni licha ya kukumbushwa mara kwa mara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mkurugenzi Mtendaji wa
HESLB Abdul-Razaq Badru na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) Prof.
Charles Kihampa wameahidi kutoa ushirikiano kwa menejimenti za vyuo ili kuhakikisha
wanafunzi wanapata mikopo kwa wakati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.