Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof. Joyce Ndalichako mwishoni mwa wiki
amekutana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali katika Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma
ambapo walizungumzia masuala mbalimbali yahusuyo Sekta ya Elimu ikiwemo
kuendeleza ushirikiano wa masuala ya
Elimu ambao umekuwepo tangu awali.
Mhe. Riziki alisema anatamani kuona walimu kutoka
Zanzibar wanapata nafasi ya kukutana na walimu wenzao kutoka bara ili waweze
kubadilishana na kupeana uzoefu wa mbinu
mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi ili kuweza kuboresha
elimu itolewayo.
‘Kuna maeneo
tofautitofauti katika kufundisha yanahitaji kutumia mbinu mbalimbali ili wanafunzi
wetu waweze kuelewa, si vibaya walimu hawa wakakutana na kubadilisha uzoefu wa
namna ya kufundisha katika maeneo hayo’ alisema Mhe. Riziki
Akizungumza katika kikao hicho cha kuimarisha
mahusiano, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Ndalichako alisema ni
vizuri kuendeleza misingi ya Ushirikiano katika masuala ya elimu ili kudumisha
Muungano wetu. Alisema Wizara ya elimu ni kubwa na inafanya kazi kwa
kushirikiana na taasisi zake ambazo zina mamlaka kisheria ikiwa ni pamoja na kutoa
miongozo kulingana na maeneo wanayoyasimamia.
Ili kwenda sambamba na kudumisha ushirikiano uliopo
baina ya Tanzania Bara na Zanzibar
Waziri Ndalichako alizitaka taasisi
za elimu zinazoshughulika na Masuala ya Muungano kutoa taarifa kwa
wakati ili kutochelewesha utekelezaji wa masuala ya elimu kwa upande wa
Zanzibar na kuleta changamoto zisizokuwa za lazima hapo baadae.
Aidha Katika kuendeleza ushirikiano kwa upande wa
walimu kupeana uzoefu, Prof Ndalichako aliliagiza Baraza la Mitihani la
Tanzania kwa kuanzia lipitie script za matokeo ya kidato cha sita kwa upande wa
Zanzibar ili kuona maeneo ambayo
wanafunzi wameshindwa zaidi ili kuweza kundaa utaratibu wa kuwakutanisha walimu
wanaofundisha masomo hayo waweze kupeana uzoefu kwa lengo la kuboresha.
Naye Naibu Waziri wa elimu Mhe. Mhandisi . Stellah
Manyanya alisema ni vizuri Wizara ikaratibu utaratibu wa watendaji wa masuala
ya kielimu kutoka Bara kukutana na wale wa Zanzibar ili kuzungumzia mambo
mbalimbali yanayoleta chanagamoto katika utekelezaji wa masuala ya kielimu kwa
lengo la kuboresha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.