Ijumaa, 19 Agosti 2016

Mamlaka ya VETA yaagizwa kufanya tathmini ya mafunzo wanayotoa


Waziri wa elimu, Sayansi naTeknolojia Mhe. Profesa, Joyce Ndalichako ametoa mwezi mmoja kwa mamlaka ya VETA kufanya tathmini ya mafunzo wanayotoa katika vyuo vyote nchini ili kuona kama yanakwenda sambamba na matakwa ya serikali ya kuwa na wataalamu watakaokwenda kufanya kazi katika viwanda.

Profesa Ndalichako ameyasema hayo alipofanya ziara leo katika Chuo cha VETA Kipawa ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake ambazo amekuwa akizifanya katika vyuo hivi ili kuona namna wanavyotekeleza majukumu yao.

Alisema katika vyuo ambavyo ametembelea amekutana na changamoto za kuwepo kwa mashine ambazo zimeachwa bila kufanyiwa ukarabati na kuwa na kutu na nyingine ni nzima lakini hazitumiki wakati vipo vyuo ambavyo havina vitendea kazi hivyo

“Ni vizuri kukawepo na usawa wa mahitaji katika vyuo vyote vya VETA kila mkoa kulingana na uhitaji na sio vyuo vingine vinakuwa na vifaa na vingine havina au vilivyopo kutotosheleza mahitaji.“ Alisema Ndalichako.

Katika hatua nyingine Profesa Ndalichako ameitaka Menejimenti ya VETA kuweka mifumo yao ya mapato vizuri ili fedha zinazopatikana kutokana na kazi wanazozifanya ziweze kuendeleza mafunzo yatolewayo katika vyuo hivyo.

Aidha, amewataka pia kuhakikisha udahili wa wanafunzi unaofanyika unaendana na ukubwa wa vyuo ili kutimiza azma ya Serikali kuwa na vijana wengi wanaopata ajira sio tu ya kuajiriwa lakini pia waweze kuajiri wengine.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Bw. Geophrey Sabuni amesema Chuo cha VETA Kipawa kinatoa mafunzo katika masuala ya Tehama, mafunzo ambayo yanalenga katika kuhudumia viwanda katika teknolojia ya juu zaidi.

Alisema matokeo ya mafunzo wanayotoa yanajidhihirisha pale wanafunzi wao wanapokwenda mafunzo kwa vitendo kwani wengi wao wanapata ajira na kushindwa kurudi chuoni hapo kumalizia mafunzo yao.


Chuo cha VETA Kipawa kinatoa mafunzo ya TEHAMA na kutoa Tuzo kuanzia ngazi ya 1 hadi 3 pamoja na stashahada ya TEHAMA.










Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.