Alhamisi, 14 Desemba 2017

Rais Magufuli asema Serikali iko tayari kulipa madai halali ya Walimu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema Serikali iko tayari kulipa madai  ya walimu ambayo wanaidai serikali endapo madeni hayo yatakuwa yamehakikiwa na kuthibitishwa kuwa ni madai halali.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Chama cha Walimu ambao unafanyika katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma Rais amesema anatambua sana shida za walimu  na kuwa serikali yake iko tayari kupatia ufumbuzi changamoto hizo.

Rais Magufuli amesema mpaka sasa tayari Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 56 kulipa madeni ya walimu na  kuwa kila mwezi  serikali imekuwa ikituma ruzuku kiasi cha shilingi bilioni 18 mpaka bilioni 23 kwa ajili ya   kuwalipa walimu.

Rais Magufuli amewataka walimu na wanafunzi  kukubali kufanya kazi katika vituo wanavyopangiwa mara wanapohitimu, Pia amesisitizia suala la mwalimu kutokuhamishwa kituo cha kazi bila kulipwa fedha yake yote na hivyo amewataka walimu kuzingatia suala hilo.

Akizungumza kabla ya Kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Ndalichako amewapongeza walimu kwa umoja na mshikamano ambao wamekuwa wakiuonyesha kupitia chama hicho cha walimu.

Chama hicho cha walimu kupitia Risala yao imeeleza kuwa inatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Tano katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya Elimu.

Katika mkutano Rais Magufuli aliwaongoza viongozi wengine kuchangisha  fedha kiasi cha shilingi milioni 60 ambazo zitagawanywa kwa walimu zaidi ya 1000 ambao wanashiriki mkutano huo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni