Alhamisi, 21 Desemba 2017

Wizara ya Elimu yaendeleza ujenzi wa Sekondari ya kumbukumbu ya Sokoine

Wizari ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kuendeleza  ujenzi wa shule ya sekondari ya kumbukumbu ya hayati Edward Moringe Sokoine inayonengwa Wilayani Mvomero mkoani Morogoro.

Akizungumza leo wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa na Wizara hiyo katika mkoa wa Morogoro Waziri Ndalichako amepongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri ya Mvomero kwa kuhakikisha inasimamia fedha zinazotolewa na Serikali kuwa zinatumika kama zilivyokusudiwa.

"Nawapongeza kwa kazi nzuri, ni jambo jema la kumuenzi hayati  Edward Moringe Sokoine kwa kuhakikisha tumekamilisha ujenzi huo ili wanafunzi waweze kuanza masomo kama inavyotarajiwa, huu ni mfano basi ni vyema na halmashauri nyingine ziige hiki ambacho Mvomero imefanya"alisema Waziri Ndalichako.

Profesa Ndalichako amesema uwepo wa shule hiyo ni kumbukumbu na pia ni kielelezo kuwa Hayati Sokoine amelitumikia Taifa hili kwa Uadilifu.

Katika ziara hiyo Waziri ametembelea kituo cha Maendeleo DAKAWA kwa lengo la kujionea hali ya Miundombinu katika shule ya Sekondari Dakawa, Kituo cha Ufundi Stadi VETA na Chuo cha Ualimu.

Pia  ametembelea Chuo cha Ufundi Stadi  VETA kilichopo Kihonda na kile kilichopo Morogoro mjini ambapo ameiagiza BODI ya  VETA kuangalia upya sifa za wakuu wa vyuo waliopo hivi sasa ili kuleta tija na ufanisi katika kazi kwani  waliopo hivi sasa hawakidhi vigezo pia hawaendani na kasi ya serikali ya awamu ya Tano.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni