Jumatatu, 9 Aprili 2018

UJENZI CHUO CHA UFUNDI NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI CHA MKOA WA KAGERA KUANZA OKTOBA 2018


Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodutus Kinawiro amesema tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa Miundombinu muhimu ya barabara na umeme katika Kijiji cha Burugo ambapo Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi stadi cha Mkoa wa Kagera kinatarajiwa kujengwa.

Kinawiro amesema hivi sasa Mkoa upo katika kukamilisha miundombinu ya maji  na kuwa tayari suala hilo limewekwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19.
Mwakilishi wa Kampuni ya ujenzi ya Kichina (CHINA QIYUAN ENGINEERING CORPORATION) Yang Tao akiwapitisha Watendaji wa Mkoa wa Kagera katika Michoro ambayo wameiandaa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Mkoa wa Kagera.


Kukamilika kwa Miundombinu hiyo kunatoa fursa ya kuanza kwa ujenzi wa chuo hicho ambapo Ujumbe wa timu ya Wataalam kutoka Kampuni ya ujenzi ya Kichina (CHINA QIYUAN ENGINEERING CORPORATION) inayotarajiwa kusimamia ujenzi wa Chuo hicho umetembelea eneo hilo ambapo umekiri kuridhishwa na hatua hizo ambazo serikali imezitekeleza.


Kwa upande wake Meneja Mkuu Msaidizi wa Kampuni hiyo Fang Kefeng amesema uwepo wa barabara, umeme na maji katika eneo la mradi utawawezesha kutekeleza ujenzi bila kikwazo  na kuwa tayari wameandaa michoro kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho na kwamba mradi utaanza mara baada Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuridhia michoro iliyoandaliwa kwa ajili ya Chuo hicho. 
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Mhandisi Enock Kayani akifafanua jambo kwa timu ya Wataalam kutoka Kampuni ya Kichina ya Ujenzi (CHINA QIYUAN ENGINEERING CORPORATION) wakati walipotembelea eneo la Mradi  katika Kijiji cha Burugo  Halmashauri ya Wilaya Bukoba Mkoani Kagera.

Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Enock Kayani amesema Mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba Mwaka huu mara baada ya Kampuni hiyo kufanya maboresho yaliyotolewa na Wizara katika michoro yao na kwamba mradi mzima utagharimu fedha za Kitanzania takribani bilioni 22 na utafanyika kwa awamu mbili.
Ujumbe wa Timu ya Wataalam kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Kichina ilipotembelea  shule ya Sekondari ya wavulana Ihungo inayojengwa upya na Serikali mara baada ya kuharibiwa vibaya na tetemekeo la ardhi lililotokea Septemba 10, 2016. Kampuni hiyo ilitembelea shule hiyo kwa lengo la kujifunza  na kuona aina ya ujenzi wa Miundombinu inayotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni