Jumanne, 17 Julai 2018

SERIKALI YAZINDUA MFUKO WA KUENDELEZA UJUZI


Serikali imezindua Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) utakaowezesha watoa huduma za mafunzo ya ufundi katika ngazi mbalimbali kutoa mafunzo yenye tija yatakayoweza kukuza stadi za kazi.

Akizindua Mfuko huo Jijini Dar es Salaam Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema mfuko huo unalenga kuboresha stadi za kazi, uwezo wa kujiajiri na kuchangia ongezeko la wataalam  wenye stadi mbalimbali katika taaluma za Kilimo, Utalii, Nishati, Ujenzi, Uchukuzi na TEHAMA.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wadau wa Elimu (hawapo pichani) waliohudhuria uzinduzi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) Jijini Dar es Salaam utakaowezesha watoa huduma za mafunzo ya ufundi katika ngazi mbalimbali kutoa mafunzo yenye tija yatakayoweza kukuza stadi za kazi uliofanyika.

Prof. Ndalichako amesema katika kuleta ufanisi wa kukuza ujuzi Wizara yake itaanzisha kwa mara ya kwanza Baraza la Taifa la Ujuzi (National Skills Council – NSC) ambalo litasimamia mabaraza ya kisekta ya kukuza ujuzi (Sectoral Skills Council).

“Tayari Wizara ina makubaliano rasmi ya ushirikiano (MoU) na Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) itakayosaidia uanzishwaji wa mabaraza hayo na  Baraza la Taifa la Ujuzi (NSC) litakuwa waangalizi wa mfuko huu wa SDF tunaouzindua leo, hivyo sekta binafsi itakuwa na fursa ya kutoa mchango wake katika ukuzaji ujuzi hapa nchini. “alisisitiza Prof. Ndalichako



Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo akizungumza na washiriki wa uzinduzi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amewataka wote watakaopata fedha za Mfuko huo kuzitumia kwa malengo yaliyowekwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dk. Erasmus Kipesha amesema Taasisi yake ina jukumu la kuusimamia Mfuko huo na imedhamiria kuhakikisha kuwa rasilimali zilizoelekezwa katika Mfuko huo zinatumika kwa weledi, taratibu, haki, ubora, na ufanisi wa hali ya juu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania Dk. Erasmus Kipesha mfano wa hundi kwa ajili ya Taasisi za Elimu ya Ufundi zitakazoshiriki katika kukuza na kuendeleza ujuzi. Makabidhiano hayo yamefanyika wakati wa uzinduzi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.