Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na uagizaji na upokeaji wa vifaa vya
maabara katika Chuo cha Ualimu Wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Waziri Ndalichako ametoa
kauli hiyo Wilayani Kasulu alipofanya ziara katika Chuo hicho na kukuta idadi
kubwa ya kemikali za maabara zisizohitajika lakini pia vifaa vya maabara
kutokuwa na ubora huku chuo kikiomba kununuliwa tena vifaa vya maabara na
kemikali.
“Haiwezekani kwa sasa
manasema mna upungufu wa vifaa pamoja na kemikali wakati mmevijaza hapa chuoni
tena kwa utaratibu usiofaa, huku mkisema vitaharibika kwa kuwa havihitajiki, ni
nani aliviagiza na ni kwanini mliviagiza bila ya kuwa na uhitaji, kwa hili sio
la kufumbia macho ni lazima hatua zichukuliwe kwa wale wote waliohusika katika
suala hili”alisema Profesa Ndalichako.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipokelewa na Mwenyekiti wa
Bodi pamoja na Watumishi wa Chuo cha Ualimu Kasulu kilichopo Mkoani Kigoma
wakati alipowasili chuoni hapo.
Waziri Ndalichako pia
ameitaka Idara ya Elimu ya Ualimu katika Wizara hiyo pamoja na Chuo cha Ualimu
Kasulu kutoa taarifa ya kina ya uagizaji na upokeaji wa vifaa hivyo kwa kuwa
kumekuwepo na kutokuelewana baina yao ni nani alitoa mahitaji halisi ya vifaa
hivyo hali iliyoisababishia Serikali hasara ya kununua vifaa visivyohitajika
wakati zipo shule za Sekondari zingeweza kupata vifaa hivyo.
“Bahati mbaya bodi yenu
haina taarifa ya manunuzi haya, wakuu wa vyuo muache tabia ya kuficha mambo
yanayoendelea chuoni hapa nachukua hatua na bodi iangalie hatua za kuchukua
hatuwezi kuruhusu mtu anayefanya uhalifu huu akabaki salama,” alisema Profesa
Ndalichako.
Wzairi wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua kemikali za Maabara
katika Chuo cha Ualimu Kasulu
Awali Mkuu wa Chuo cha
Ualimu Kasulu Josephat Mwangamila katika hotuba yake alisema Chuo hicho kina
deni la takribani shilingi milioni 64 kwa ajili ya ununuzi wa Kemikali na Vifaa kwa
ajili ya matumizi ya ofisi (stationary) kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha
sita waliofanya mitihani.
Mkuu wa Chuo alisema
walifikia uamuzi wa kununua kemikali hizo kwa kuwa hawakuwa nazo chuoni hapo
lakini pia zilizokuwepo hazihitajiki kwa matumizi chuoni hapo.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya majengo
ya Chuo Cha Ualimu Kabanga Mkoani Kigoma. Akiwa Chuoni hapo Profesa Ndalichako
amezungumza na wakufunzi pamoja na watumishi wa chuo na kuahidi kujenga upya
Chuo hicho kwa kuwa miundombinu yake imechakaa.
Serikali imenunua vifaa vya
maabara vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni Moja ambavyo vimesambazwa katika vyuo vyote vya ualimu nchini ikiwa ni
juhudi za kuhakikisha walimu wanapata mafunzo kwa vitendo ili wakaweze kufundisha
kwa umahiri pindi wanapomaliza masomo yao.
Waziri wa Elimu pia
ametembelea Chuo cha Ualimu Kabanga ambapo ameahidi kujenga upya chuo hicho
katika mwaka wa fedha ulioanza 2018/19 kwa kuwa majengo yake ni chakavu na
kuvitaka vyuo ambavyo vimekarabatiwa kuwa na dhamira ya dhati ya kutunza
miundombinu ya vyuo.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya ngazi za
mabweni ambayo imechakaa katika Chuo Cha Ualimu Kasulu, Wilayani Kasulu Mkoani
Kigoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.