Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave Maria
Semakafu amewataka walimu wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu kuacha
vitendo vya unyanyapaa kwa wanafunzi hao, kwa kuwa taaluma waliyonayo inahitaji
upendo na uvumilivu.
Dk. Semakafu ametoa kauli hiyo
mkoani Mwanza wakati akizungumza na walimu hao ambao wanashiriki mafunzo maalumu
ya siku 10 ya kuchambua mtaala ulioboreshwa wenye lengo la kuwajengea uwezo
walimu wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wa akili, wasioona na wanafunzi
viziwi.
Naibu Katibu Mkuu akizungumza na walimu wanaoshiriki mafunzo ya
kuchambua mtaala ulioboreshwa yanayofanyika katika Chuo Cha Ualimu Butimba
mkoani Mwanza
Dk. Semakafu amesema pamoja na
mambo mengine amewataka walimu kuacha masuala ya vitengo na badala yake walimu
wafanye kazi zao kwa weledi, ikiwa ni pamoja na kuwa wanaharakati katika masuala
ya Elimu.
“Walimu naomba niwaambie ukweli
huko kwenye shule zetu tumeanzisha vitengo ambavyo havina sababu yoyote na
tumekuwa hatufanyi kazi zetu kwa weledi, wengine hatufundishi kwa visingizo vya
kuwa tunasimamia vitengo, tuache mara moja na badala yake tufundishe watoto
wetu kwa weledi,” alisisitiza Dk. Semakafu.
Walimu wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu
wakifuatilia mafunzo ya kuchambua mtaala mpya ulioboreshwa mkoani mwanza.
Katika mafunzo hayo baadhi ya
Walimu walitaka kufahamu kuhusu suala la wanafunzi kuishia Darasa la Sita
ambapo Dk. Semakafu alieleza kuwa Elimu inaongozwa na Sheria na Sheria yetu ya
Elimu Msingi ni miaka Saba hivyo Sheria ya Elimu haijabadilika.
Mafunzo hayo yanashirikisha
walimu 132 wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu kutoka mikoa wa
Kagera, Geita, Kigoma, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Rukwa na Tabora.
Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave Maria Semakafu akikagua vifaa katika
maabara ya Baiolojia katika Chuo Cha Ualimu Butimba, mkoani Mwanza
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.