Ijumaa, 17 Agosti 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA ARIDHISHWA NA UKARABATI WA CHUO CHA UALIMU NACHINGWEA


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha ametembelea Chuo Cha Ualimu Nachingwea na kuridhishwa na kiwango cha ukarabati kinachoendelea ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kimetolewa kwa ajili ya ukarabati huo. 

Akizungumza na watumishi katika Chuo hicho Naibu Waziri Ole Nasha amepongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha sita kwa mwaka 2018 kwa mkoa wa Lindi kushika nafasi ya pili Kitaifa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na Wazazi pamoja na Walimu (hawapo pichani) wa Shule ya Sekondari Nachingwea Mkoani Lindi mara baada ya kufanya ziara shuleni hapo. 

Naibu Waziri pia amewataka walimu kuhakikisha wanasimamia, wanahamasisha na kuelimisha jamii kuachana na  mila na desturi potofu zinazochangia watoto kuacha shule ikiwa ni pamoja na kushiriki katika unyago.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole Nasha ametembelea na kuipongeza Halmashauri kwa kuwa na wazo la kuwa na Shule ya Sekondari ya wasichana Nachingwea na kuwa hiyo itasaidia watoto wa kike kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiwa na Viongozi mbalimbali wa Chuo cha Ualimu Nachingwea Mkoani Lindi akikagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara mara baada ya kupokelewa Chuoni hapo.

Mheshimiwa Ole Nasha amesema wazazi na wadau wana wajibu wa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vinavyowanyima fursa, ambapo amewataka Walimu kuhakikisha wanasimamia wanafunzi ili waweze kufikia malengo yao.

Naibu Waziri ameahidi kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa viwili na nyumba 2 za walimu ili kupunguza changamoto za shule hiyo.
Muonekano wa Jengo la darasa lililokarabatiwa katika Chuo cha Ualimu Nachingwea Mkoani Lindi. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameridhishwa na namna ukarabati wa jengo hilo ulivyofanyika.  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni