Ijumaa, 14 Desemba 2018

BILIONI 51 KUTUMIKA KUUENDELEZA ELIMU YA UFUNDI NCHINI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amepokea nakala ya mkataba wa mradi wa kuendeleza ajira na Elimu ya Ufundi kutoka  serikali ya Italia wenye lengo la kuviwezesha vyuo vinavyotoa mafunzo hayo nchini.

Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam katika ofisi ndogo za Wizara hiyo kupitia Balozi wa Italia nchini Roberto Mengoni ambapo waziri Ndalichako ameahidi kufanya ufatiliaji wa karibu kuhakikisha mkataba huo unasainiwa haraka ili kuwezesha kuanza kwa mradi huo.

Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea nakala ya mkataba wa kuendeleza ajira na Elimu ya Ufundi kutoka kwa Balozi wa Italia nchini Roberto Mengoni, makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.

Waziri Ndalichako amesema mradi huo ni wa miaka mitano utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 51 na utazihusisha  Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), naTaasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KISS) kushiriki kikamilifu kuchangia katika kufanikisha malengo ya Taifa ya ukuaji wa uchumi .

Aidha, Waziri ndalichako amesema kuanzishwa kwa mradi huo kutavisaidia vyuo kupata vifaa vya kisasa na miundombinu kuboreshwa na hatimaye utoaji wa elimu bora ya ufundi kwenye taasisi shiriki hasa elimu ya vitendo itakayowapa wanafunzi ujuzi utakao wawezesha kujiajiri.
Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa na Balozi wa Italia nchini Roberto Mengoni wakijadili na kubadilishana mawazo mara baada ya kumaliza kusoma vipengele vya nakala ya mkataba wa kuendeleza ajira na Elimu ya Ufundi wakati wa makabidhiano ya nakala hiyo yaliyofanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika makabidhiano hayo Balozi Roberto Mengoni amesema serikali ya Italia kupitia ubalozi wa nchi hiyo tayari imetuma  mtaalam wake Marcella Ferracciolo kufanya maandalizi ya utekelezaji wa mradi ambapo mpaka sasa mtaalamu huyo ameshatembelea taasisi zote zinazotarajiwa kutekeleza mradi huo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni