Ijumaa, 14 Desemba 2018

DKT. AKWILAPO: SEKTA YA ELIMU INA MAFANIKIO MAKUBWA KWA SASA


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amesema Serikali ya awamu ya Tano ya inatambua mchango na juhudi zinazofanywa na shule zinazoendeshwa na makanisa hapa nchini (CSSC) ikiwa ni pamoja na baadhi ya shule kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani na kutoa malezi bora kwa watoto.

Dkt. Akwilapo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wakuu wa Shule za Sekondari za Makanisa na kueleza kuwa mafanikio ambayo yamepatikana katika sekta ya elimu hivi sasa ni makubwa ukilinganisha na wakati nchi inapata uhuru.
Wakuu wa shule za Sekondari za Makanisa  hapa nchini wakimsikiliza Katibu Mkuu (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano wenye lengo la kujadili mafanikio na Changamoto katika shule wanazozisimamia.mkutano huo wa siku mbili unafanyika mkoani Dodoma.

Ameeleza kuwa  Wakati nchi inapata uhuru mwaka 1961 kulikuwa na  shule 3,238  lakini hadi kufikia mwaka 2018  zipo  shule za elimu ya  msingi 17,704 zilizosajiliwa , Elimu ya sekondari zilianza shule 41, lakini sasa kuna  shule  4,963 zilizosajiliwa   na kati ya hizi  shule  1,266   ni shule binafsi.

Vyuo vya ualimu navyo vimeongezeka kutoka vyuo 3 Lakini sasa kuna vyuo 138  na  kati ya hivyo   103 viko chini ya umiliki wa taasisi binafsi  ambapo  makanisa  wanamiliki  vyuo  15.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akizungumza na Wakuu wa shule za Sekondari za Makanisa wakati akifungua mkutano huo na kueleza kuwa Sekta ya elimu imekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya Tano ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu mbalimbali katika sekta hiyo.

“Nawapongeza kwa kutoa huduma na kusimamia elimu, zipo baadhi ya shule zenu ni mfano  katika kufanya vizuri kwenye matokeo, shule za makanisa  pia zinatoa malezi bora kwa watoto kwa lengo la kuwa na viongozi bora na waadailifu wa Taifa la baadae, hii ni juhudi ya kuunga mkono serikali ya awamu ya Tano na serikali yenu inatambua hilo,”alisistiza Dkt. Akwilapo.

Kwa upande wake Mwalimu Petro Masatu ambaye ni Mkurugenzi wa huduma  za elimu CSSC alimweleza Katibu Mkuu baadhi ya changamoto walizonazo ikiwa ni pamoja na suala la upimaji wa watoto /wanafunzi kwa kuzingatia umahiri kutoka darasa moja kwenda jingine kuwa bado kuna utata kati ya shule zisizo za serikali, Wazazi na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuchelewa kwa Sekula mpya kwa shule zisizo za serikali ili uwe mwongozo mzuri kwa mwaka 2019 pamoja na kuchelewa kwa sheria mpya ya elimu ambayo yote Katibu Mkuu ameahidi kuyafanyia kazi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akisalimiana na baadhi ya viongozi wa CSSC muda mfupi baada ya kupokelewa na wenyeji wake katika mkutano wa Wakuu wa shule za sekondari za makanisa unaofanyika mkoani Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni