Jumatano, 5 Desemba 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA ASEMA SERIKALI IMEJIZATITI KUIMARISHA ELIMU NCHINI


Serikali ya awamu ya Tano imesema miongoni mwa vipaumbele vyake ni pamoja na kuimarisha na kuboresha Elimu nchini na ndiyo maana sekta hiyo imetengewa fedha nyingi katika bajeti ya Taifa.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha mkoani Morogoro wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wanaosimamia Elimu katika mkoa huo na kueleza kuwa kwa sasa Tanzania ni nchi inayosifiwa kwa kuongeza bajeti ya Elimu kwa asilimia 21.4 ya bajeti ya jumla ya Taifa.
 
“Ninachoweza kusema kwa sasa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka inapokea bajeti yake ambayo ni sh trilioni 1.4 na kwenye fedha za Maendeleo zinapatikana zote kwa asilimia 100 kwa ajili ya kutekeleza shughuli za Elimu bila kuchelewa yote haya ni kwa sababu Sekta ya Elimu ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano,” aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha akiongea na viongozi wa elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mara baada ya kuwasili katika Halmashauri hiyo kukagua miradi ya Elimu.

 Amesema katika miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kumefanyika uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya Elimu kuliko wakati wowote na kuwataka watendaji wa sekta hiyo kusimamia fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya Maendeleo ya Elimu kwa umakini ili kuweza kubadilisha mazingira ya watoto ya kujifunzia.

 “Wote ni mashahidi kuhusu ujenzi wa miundombinu ya Elimu inayoendelea nchini, Juzi mmeona Mhe.  Rais John Magufuli akifungua maktaba kubwa kuliko maktaba zote Afrika Mashariki na Kati, maktaba yenye uwezo wa kuchukua vitabu laki nane na wanafunzi 2,100 kwa wakati mmoja lakini pia kwenye vyuo vya ufundi na shule pia kuna uwekezaji mkubwa ambao umefanyika wa kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia vyote hivyo ni kwa sababu sekta ya Elimu ni kipaumbele,” alisisitiza Ole Nasha
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha akikagua mradi wa ujenzi ya sekondari ya Kumbukumbu ya Sokoine inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro. Yanayoonekana hapo ni madarasa ambayo yatakuwa katika mfumo wa ghorofa. 

Naibu Waziri Ole Nasha yuko mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi ya siku tatu na kuwa ziara hiyo inatarajiwa kuhitimishwa leo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha akikagua majengo ya Chuo cha Ualimu Ilongo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ambayo miundombinu yake imefanyiwa ukarabati na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya EP4R.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni