Ijumaa, 14 Desemba 2018

SERIKALI YATOA MAELEKEZO UJENZI WA VETA SIMANJIRO


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia WilliamOle Nasha ameitaka Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara kuhakikisha inahusisha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA katika ujenzi wa Chuo Cha VETA Wilayani humo ili miundombinu ya chuo hicho ijengwe kwa utaratibu na viwango vinavyohitajika.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo Mkoani Manyara wakati akikagua eneo ambalo Serikali ya Wilaya hiyo inategemea kujenga Chuo cha Veta kwa kushirikiana na Shirikala Maendeleo ya Hiari ECLAT.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Yefred Myenzi kuhusu namna walivyojipanga kujenga Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Wilaya katika eneo la Mradi la Emboreet lililoko katika Wilaya hiyo.
Alisema ni vizuri Mamlaka husika zikahusishwa katika ujenzi wa Chuo hicho kuanzia hatua za awali na kumtaka Mkurugenzi wa kanda  hiyo na yule wa Mkoa kufika katika eneo la Emboreet ambako mradi utajengwa ili kuzungumza  na wananchi ili mradi utekelezwe kwa utaratibu  unaostahili.

“Mnataka kujenga chuo cha Ufundi ni wazo zuri lakini ni lazima kijengwe kwa utaratibu sio kiholela kwa sababu kumeanza kuibuka utitiri wa vyuo ambapo mtu anakuwa na jengo moja anakutana chuo, kuna viwango na masharti ambayo ni lazima yatimizwe kabla chuo kuruhusiwa kufanya kazi kwa hiyo na nyinyi fuateni taratibu hizo ili muweze kuanzisha chuo cha Ufundi,” alisisitiza Naibu Wazizri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akitoa zawadi kwa mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Kitwai A aliyefanya vizuri katika mitihani ya kuhitimu darasa la saba mwaka 2018. Shule ya Msingi Kitwai A imefaulisha wanafunzi 25 kati ya 28 waliofanya mtihani mwaka huu. 
Mheshimiwa Ole Nasha amesema Serikali ya Awamu ya Tanoimeweka mkazo mkubwa katika Elimu ya Ufundi kwa kuwa kuna vijana wengi wanaomaliza shule wanaishia kutokuwa na ajira kwa kuwa hawana maarifa yanayowasaidia kupata ajira hasa pale wanapokosa fursa ya kuendelea na elimu ya juu hivyo ujenzi wa vyuo vya ufundi vingi utasaidia kuwajengea vijana  uwezo wa kujiajiri.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Yefred Myenzi alisema wazo la kuanzisha  kwa Chuo hicho kutawawezesha vijana  kupata maarifa ya kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.

Naye Meneja Mradi ya ECLAT Bakiri Angalia alisema  pamoja na shirika hilo kushiriki ujenzi wa Chuo hicho  pia  imefadhili miradi ya Elimu yenye thamani ya  zaidi ya sh bilioni 3 katika Wilaya hiyo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiongea na wakazi wa Kata ya Kitwai A iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara ambapo amewataka kuhakikisha wanawandikisha shule wanafunzi wote wenye umri wa kuanza shule bila kuwaacha nyumbani na kuwapangia majukumu mengine.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni