Jumanne, 18 Desemba 2018

KATIBU MKUU DKT. AKWILAPO AWATAKA WATENDAJI WA WIZARA YA ELIMU KUBORESHA UTOAJI HUDUMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt.  Leonard Akwilapo amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuboresha utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wadau wote wanaofika  katika Wizara hiyo.


Dkt. Akwilapo ameyasema hayo leo mkoani Morogoro wakati akifungua Semina ya Mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu kwa baadhi ya Maafisa wa Wizara hiyo lengo likiwa ni kuwakumbusha Maafisa namna bora ya utoaji wa huduma ili kuleta ufanisi na tija wakati wa kuwahudumia wadau.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo (Hawapo pichani) wanaohudhuria mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu kwa Maafisa wa Wizara hiyo, mafunzo hayo yanafanyika mkoani Morogoro.

Dkt. Akwilapo amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina idara na vitengo hivyo amewataka watendaji wote kuzingatia kanuni, taratibu za za utumishi muda wote wanapokuwa wanawahudumia watu kutoka nje ya ofisi hiyo.

"Utumishi wa umma una maadili yake, sasa ni vyema mkayazingatia wakati mnapokuwa mnatekeleza majukumu yenu katika kuwahudumia wananchi, tumieni lugha nzuri na mhakikishe mteja anaridhika naamini kuwa baada ya mafunzo haya nahitaji kuona mabadiliko katika kuhudumia wateja na huduma anayopewa mteja ili kuepuka malalamiko,”alisisitiza Dkt. Akwilapo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Raslimali Watu Sebastian Inoshi akizungumza na Watumishi wa Wizara hiyo (Hawapo Pichani) kuhusu Mafunzo ya Huduma kwa Wateja na Utunzaji wa Kumbukumbu.

Mafunzo hayo ni utekelezaji wa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 toleo la tatu kifungu cha G 20 kinachoelekeza mtumishi kupatiwa mafunzo kazini ili kuboresha utendaji kazi wake.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Raslimali Watu Sebastian Inoshi amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara kwa  kuwakumbusha umuhimu wa huduma kwa wateja na utunzaji wa kumbukumbu ili kuwawezesha kufanya kazi kwa weledi.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leornad Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wanaoshiriki mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu kwa Maafisa wa Wizara hiyo yanayofanyika mjini Morogoro

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.