Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameziangiza taasisi zote zinazotoa
Elimu ya Mafunzo ya Ufundi zilizo chini ya Wizara hiyo kuwafundisha wanafunzi
kwa vitendo ili kuwawezesha wanafunzi hao wawe wabunifu na waweze kujiajiri.
Waziri Ndalichako
ametoa agizo hilo wakati wa Mahafali 12 ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam
yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam ambapo amekagua miradi mbalimbali
iliyobuniwa na wanafunzi wa taasisi hiyo pamoja na kuzindua jengo la mradi wa
wanafunzi linalojengwa na wanafunzi kupitia mafunzo kwa vitendo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.
Joyce Ndalichako akimkabidhi mfano wa hundi mmoja wa wanafunzi wa Taasisi ya
Teknolojia Dar es Salaam aliyeshinda katika kuandaa mradi wa ubunifu wakati
wakati wa Mahafali ya 12 ya Taasisi hiyo.
Waziri Ndalichako
amesema lengo la serikali kutoa Mafunzo ya Ufundi ni kwa ajili ya kuwaandaa
wanafunzi kwa kuwapa ujuzi utakaowasaidia kutatua changamoto zilizopo katika
Jamii na kuwawezesha kuchangia katika ukuaji kwa uchumi nchini pamoja na
kushiriki katika kujenga uchumi wa viwanda.
"Nimepata fursa
ya kutembelea miradi mbalimbali iliyobuniwa na kutengenezwa na wanafunzi wakati
wa mafunzo kwa vitendo inatia moyo kwani bunifu zote zimelenga kutatua matatizo
yaliyopo katika jamii." alisema Waziri Ndalichako
Waziri Ndalichako pia
amewataka wahitimu hao kuwa na nidhamu wanapokwenda kwenye soko la ajira na
kuhakikisha bunifu zao zinawafikia wananchi na kutatua changamoto zilizopo
badala ya kuishia katika maonesho.
Akizungumza katika
Mahafali hayo Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Preksedis Ndomba amesema Taasisi ya DIT
inajivunia bunifu mbalimbali ambazo taasisi hiyo imezibuni, pia zimesaidia kuondoa kuondoa changamoto katika Jamii ikiwemo mradi
wa taa za barabarani ambazo zimewekwa katika baadhi ya mikoa ikiwemo Simiyu na
Dar es Salaam.
Kabla ya kushiriki
sherehe za Mahafali hayo Waziri Ndalichako alizindua jengo la mradi wa
wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam wanalojenga kupitia mafunzo
kwa vitendo.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizindua jengo la mradi
wa wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam wanalojenga kupitia mafunzo
kwa vitendo wakati wa Mahafali ya 12 ya Taasisi hiyo iliyofanyika jijini Dar es
Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.