Ijumaa, 14 Desemba 2018

WAZIRI NDALICHAKO AAHIDI KUSHUGHULIKIA UCHAKAVU WA MIUNDOMBINU VYUO VYA VETA NCHINI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameahidi kushughulikia changamoto ya uchakavu wa miundombinu katika vyuo vya ufundi stadi vinavyomilikiwa na VETA ili vyuo hivyo viweze kutoa mafunzo bora yanayoendana na Teknolojia ya kisasa.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati wa sherehe za mahafali ya 33 katika Chuo Cha VETA kilichopo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro na kusisitiza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na  Teknolojia ina jukumu la kuhakikisha Taasisi   zilizo chini yake zinakuwa  na mazingira bora  ya kazi , hivyo  iko tayari kupokea mchanganuo wa mahitaji ya vyuo vya ufundi stadi nchini ili vyuo hivyo viweze kufanyiwa kazi.

“Wizara ikiwezeshwa  vizuri ikafahamu mahitaji ya vyuo hivi vya Ufundi Stadi na kwa sababu ni kipaumbele cha serikali ya awamu ya Tano katika kuwezesha nchi kuwa na uchumi wa kati basi tuko tayari kupokea ushauri  wa wataalam ili tuweze kuhakikisha kuwa tunaimairisha mafunzo ya ufundi stadi kwa kiwango ambacho ndio kinahitajika na wataalam na wajiri pindi vijana wanaoomaliza mafunzo,” alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako  akisikiliza maelezo kutoka kwa mhitimu  wa fani ya kukaanga Mvuke kwenye  maonesho ya Mahafali ya 33 Chuoni hapo. Aliyesimama kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu.

Waziri Ndalichako amesema kuwa  mfumo wa mafunzo kwa njia ya uanagenzi una manufaa siyo tu  kusaidia kuongeza udahili,  lakini pia mfumo huu unasaidia vijana kujifunza teknolojia mpya zilizopo viwandani, kusaidia vijana kupata ujuzi na uzoefu halisi unaohitajika mahala pa kazi katika fani husika na makampuni kuwa na uhakika wa nguvukazi yenye umahiri wa kiwango wanachokihitaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi - VETA- Dkt. Pancras Bujulu alisema kuwa baadhi ya vyuo vya VETA ni vikongwe mno na miundombinu yake imechakaa  na vinahitaji ukarabati.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akitazama nyaraka za kampuni ya LES Inspection iliyoanzishwa na wahitimu wa VETA ambao wamefuzu na kupata leseni za kutoa ithibati ya kazi za uungaji vyuma kwa kiwango cha kimataifa wakati akitembelea maonesho ya mahafali ya 33 ya Chuo cha VETA katika manispaa ya Moshi.

Dkt. Bujulu alimweleza Waziri Ndalichako kuwa pamoja na uchakavu wa Miundombinu lakini pia  vifaa na mashine zinazotumika kwenye karakana kwa ajili ya kufundishia nazo  zimechakaa na zingine  zimepitwa na wakati kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia hivyo hazifai kutumika kufundishia, vifaa vinavyohitajika ni vile vinavyoendan na Teknolojia.

Jumla  ya wahitimu 174 wa fani mbalimbali  wamehitimu mafunzo yao katika mahafali hayo ya 33 katika Chuo hicho Cha VETA, manispaa ya Moshi mkoani  Kilimanjaro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni