Ijumaa, 14 Desemba 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA ASHIRIKI UJENZI WA SHULE WILAYANI SAME


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.William Ole Nasha ameshiriki shughuli za ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Ruvu iliyopo Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.

Mhe.Ole Nasha ameshiriki ujenzi huo na Wananchi wa Kijiji cha Ruvu Darajani wakati kukagua miradi ya inayotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia katika Wilaya hiyo ambapo amewataka wananchi kuendeleza jitihada hizo ili kuweka  mazingira mazuri ya wanafunzi kusoma.
Naibu Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akishiriki ‘Msaragambo’ wa Ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Ruvu iliyoko Kata ya Ruvu Darajani Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro alipofanya ziara kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa katika Wilaya hiyo.

Kufuatia jitihada hizo za Wananchi Naibu Waziri Ole Nasha amewaahidi wananchi kuwa Wizara itajenga  vyumba viwili vya madarasa, mabweni mawili na matundu ya vyoo ikiwa ni kuunga mkono juhudi ambazo wananchi wa kijiji cha Ruvu Darajani wameonesha lakini pia kuwezesha wanafunzi kutulia shuleni na kusoma.

“Serikali ikiona eneo ambalo wananchi wameanza na wana hamasa ya kujiletea maendeleo haiwezi kusita kuja kusaidia, Wilaya ya Same mmeonesha mfano kupitia utaratibu wenu wa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano hivyo Wizara itaunga mkono juhudi hizi kwa kuwajengea vyumba vya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akitoa aelekezo katika eneo ambalo vyumba viwili vya madarasa vitajengwa katika Shule ya Msingi Ruvu Iliyoko katika Kata ya Ruvu Darajani Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.

Naibu Waziri huyo pia amewataka wananchi wa Kijiji cha Ruvu Darajani ambao wanajihusisha na shughuli za ufugaji kuacha kutumia watoto kuchunga mifugo badala yake kuhakikisha wanatumia fursa ya Elimu bure kuwaandikisha watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Staki alimweleza Naibu Waziri wa Elimu kuwa changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Ruvu ambayo imetokana na ongezeko la Wanafunzi waliohamishiwa shule hiyo kutokana na shule walizokuwa wakisoma miundombinu yake kuathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua za masika za mwaka huu.

Katika ziara hiyo Naibu Waizri Ole Nasha pia alitembelea shule ya Sekondari Makanya, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same na Shule ya Sekondari Same ambapo ameridhishwa na ukarabati ulivyofanyika katika shule kongwe hiyo .
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua ukarabati wa miundombinu uliofanyika katika Shule ya Sekondari Same iliyoko Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro. Ameridhishwa na namna ukarabati huo ulivyofanyika na kuwataka kutunza miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni