Ijumaa, 21 Juni 2019

NAIBU WAZIRI OLE NASHA ATAKA WATOTO KULINDWA NA KUWEZESHWA ILI WAWEZE KUSHIRIKI FURSA MBALIMBALI ZA ELIMU

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amesema Serikali  inatambua  na kuthamini umuhimu wa mtoto wa kitanzania na ndio maana imekuwa ikizifanyia kazi haki za msingi za mtoto ili aweze kuishi katika mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na kupata elimu. 

Naibu Waziri Ole Nasha ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyoandaiwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) ambapo amesema watoto wanapaswa kulindwa na kuwezeshwa ili waweze kushiriki katika  fursa mbalimbali zilizopo kwenye elimu. 


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afirika yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam Juni 20, 2019.
 Amesema maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yanatoa fursa ya kujadili changamoto na fursa katika kuhakikisha kuwa haki za mtoto zinalindwa na kwamba  Serikali imefanya jitihada kubwa na za makusudi katika kuhakikisha kuwa watoto wanapata haki zao za msingi katika jamii zetu za kitanzania.


Ole Nasha amezitaja jitihada hizo kuwa ni pamoja na kuridhiwa kwa mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayolinda haki za watoto, kutunga  sheria zinazolinda haki za watoto dhidi ya uonevu na ubaguzi wowote na pia imepitisha Sera zinazowalinda na kuwapatia fursa watoto.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akichangia mjadala wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Jitihada nyingine ni pamoja na ujenzi wa shule karibu na makazi ya watu ili kupunguza watoto kutembea umbali mrefu, ujenzi wa mabweni na pia  mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka mkazo juu ya stadi za maisha, elimu ya afya ya uzazi na ujinsia katika shule za msingi na sekondari na vyuo vya ualimu.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole Nasha ameutaka umma kutambua kuwa jukumu la kuwaendeleza watoto kielimu ni la kila mmoja wetu na kwamba ifahamike kuwa watoto wa kike na wa kiume wote ni sawa, hivyo hatuna budi kuwapunguzia watoto wa kike mzigo wa kazi za nyumbani ili wapate muda wa kujisomea sawa na ilivyo kwa watoto wa kiume.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipokea risala kutoka kwa mmoja wa watoto walioshiriki Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Jijini Dar es Salaam.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa Juni 16 ya kila mwaka ambapo kwa mwaka 2019 maadhimisho hayo Kitaifa yamefanyika Mkoani Geita na yalikuwa na Kauli Mbiu isemayo “Mtoto ni Msingi wa Taifa Endelevu: Tumtunze, Tumlinde na Kumuendeleza.”

NDALICHAKO AZINDUA MABARAZA YA UJUZI YA KISEKTA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema serikali kupitia Wizara ya Elimu inaendelea kuimarisha stadi na ujuzi katika sekta sita za kipaumbele ili kufikia azma ya kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo 2025.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati wa halfa ya uzinduzi wa Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta jijini Dar es Salaam ambapo mabaraza hayo yaliyoundwa kupitia Mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ) na sekta zilizopewa kipaumbele katika Mpango Mkakati wa Taifa wa Kukuza na Kuendeleza ujuzi ni pamoja na Kilimo, TEHAMA, Nishati, Ujenzi, Uchukuzi na Utalii.

“Katika azma ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo 2025, tunapaswa kuhakikisha nchi  yetu inakuwa na nguvukazi yenye ujuzi na stadi stahiki zinazohitajika kwenye soko la ajira,” amesisitiza Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta Prof. Ndalichako amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliingia makubaliano rasmi ya ushirikiano (MoU) na Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) ili kusimamia uanzishaji na kuratibu mabaraza hayo ambayo yatakuwa kiunganishi muhimu kwa kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa masuala ya kuendeleza na kutumia ujuzi nchini.

“Tutaendelea kutoa ushirikiano kwa sekta binafsi na wadau wengine kwa kuweka mifumo wezeshi na rafiki, programu mbalimbali za kuendeleza ujuzi, na kuimarisha miundombinu ili kuhakikisha nchi inajenga ujuzi na stadi stahiki kwa ustawi wa maendeleo ya nchi,” amesema Prof. Ndalichako.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte, akitoa hotuba ya utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako kufungua rasmi Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta.
Waziri Ndalichako amesema kupitia ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Umma serikali inatarajia kupata ushirikiano katika programu za mafunzo ya wahitimu tarajali mahali pa kazi (internships) na kutambua ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu (recognition to prior learning - RPL) ili kupunguza na kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.

Aidha, Prof. Ndalichako ametoa ombi kwa sekta binafsi kuendelea kupokea vijana wanaokwenda kufanya mafunzo kwa vitendo ili kuwajengea utayari wa kuingia kwenye soko la ajira.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akisalimiana na wadau waliohudhuria katika uzinduzi rasmi wa Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Salum Shamte alisema mabaraza yatakuwa ni fursa pekee ya kuunganisha Taasisi Binafsi, Serikali na Wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka nje ya nchi katika kuleta ufanisi katika maendeleo.

Shamte amesema TPSF imekuwa ikitoa ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa serikali kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) katika ngazi ya wilaya, Mkoa , Wizara na hata Taifa ili yaweze kufanyiwa kazi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akipongezwa na Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte mara baada kuzinduzia Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Sekta ya Kilimo akitoa neno la shukrani.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Sekta ya Kilimo.

Wadau wa Sekta ya Nishati wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.
Wawakilishi kutoka Sekta ya Tehama wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako.

Wawakilishi kutoka TEA na Bodi ya Mikopo wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa wanafunzi wa Vyuo Vikuu.

Washirika wa Maendeleo wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Sekta ya Utalii.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Sekta ya Usafirishaji.